VIDEO: Viporo kugharimu Sh 417 milioni

Friday May 22 2020

By Edwin Mjwahuzi

Mechi 93 za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobakia kabla haijafikia tamati, zitagharimu zaidi ya Sh 417 milioni.
Kiasi hicho cha fedha ni gharama za uendeshaji kwa timu na malipo ya posho kwa waamuzi na maofisa wengine wanaosimamia michezo ya Ligi Kuu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa tathmini iliyofanywa na timu ya wataalam wa wizara yake imeonyesha kuwa kiwango hicho cha fedha kinahitajika ili kuweza kumalizia ligi hiyo iliyobakiza raundi 9.
Alisema kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), klabu pamoja na wadhamini wanalo jukumu la kuona wanamudu vipi gharama hizo.
"Kwa kweli gharama za uendeshaji ni kubwa zaidi ya Sh 417 milioni gharama za jumla. Gharama hizi za posho na mishahara ya wachezaji.
Kwakweli tumekubaliana na mimi niliridhia kwamba zitakuwa chini ya TFF, Bodi ya Ligi na klabu zenyewe kupitia wadhamini wa ligi hizo ambazo ni Vodacom, Azam na wadhamini binafsi wa klabu hizo," alisema Waziri Mwakyembe.
Idadi ya mechi kwa raundi tisa (9) zilizobakia jumla ni 89 lakini pia kuna nyongeza ya michezo minne (4)
 ambayo inatokana na baadhi ya timu kucheza mechi pungufu.
Wakati idadi kubwa ya timu zikiwa zimecheza mechi 29 kila moja, Yanga imecheza mechi 27 tu wakati Simba, Azam FC,Namungo FC, Coastal Union, Ruvu Shooting na Mwadui kila moja ikiwa imecheza mechi 28.
Tanzania Prisons yenyewe ndio timu iliyocheza idadi kubwa ya mechi hadi wakati ligi hiyo iliposimama ambapo ilikuwa imeshacheza mechi 30.

Advertisement