VIDEO: Takukuru yajitosa kumsaka Hans Poppe

Friday September 14 2018

 

By Ibrahim Yamola

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemtaka Zacharia Hans Poppe kuripoti katika ofisi za taasisi hiyo au polisi kujibu tuhuma zinazowakabiri.

Mbali na Hans Poppe mwingine ni Franklin Lauwo ambaye naye anatakiwa kujisalimisha.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo akizungumza leo Septemba 14, 2018 amesema Zacharia alitoa taarifa za uongo kuhusu malipo ya kodi.

Amesema Zacharia kwa kushirikiana na washtakiwa wengine Evans Aveva, Geofrey Nyange 'Kaburu' walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba Klabu ya Simba wamenunua nyasi bandia kutoka kampuni ya Ninah Guangzhou Trading Company kwa thamani ya dola za Marekani 40,577, maelezo ambayo yalikuwa ya uongo kwani nyasi hizo zilinunuliwa kwa dola 109,499.

Kuhusu Lauwo, Mbungo amesema alifanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Simba uliopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa Sh249, 929,704 wakati akiwa hajasajiliwa katika Bodi ya Makandarasi Tanzania.

"Tumewatafuta kwa njia za siri na uwazi bila mafanikio. Tunawataka kuripoti kituo cha Takukuru au polisi," amesema Mbungo

"Mwananchi atakayefanikisha kupatikana kwa watu hawa atapatiwa zawadi."

Amesema kwa taarifa walizonazo, Zacharia aliondoka nchini akaenda Mombasa-Kenya, "Kisha akaenda nchi zingine na kuna taarifa yupo hapa nchini amejificha. Tunamtaka yeye na mwenzake wajisalimishe. "

Naibu Mkurugenzi huyo amesema katika uchunguzi, Zacharia ameonekana kuwa na passpoti tatu tofauti ambazo ni Afrika Mashariki na mbili za Tanzania zenye namba tofauti.

Advertisement