VIDEO: Simba wakimataifa waifuata AS Vita

Muktasari:

Simba imeondoka bila nahodha wake, John Bocco ambaye alipata majeraha kwenye mchezo uliopita.

Dar es Salaam.  Timu ya Simba imeondoka leo Alhamisi asubuhi kkwenda nchini DR Congo kwa ajili ya mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya As Vita keshokutwa Jumamosi.
Simba imeondoka bila nahodha wake, John Bocco ambaye alipata majeraha kwenye mchezo uliopita.

Timu hioyo imesafiri na Shirika la Ndege la Kenya KQ na inatarajia kufika Kinshasa saa 7 mchana sawa na  saa 9 kwa hapa nchini.

Wekundu wa Msimbazi wameondoka wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi yao ya kwanza hatua ya makundi baada ya kuifunga JS Saoura mabao 3-0.

Simba siyo wageni kwenye Uwanja wa Martyr kwa sababu walicheza uwanjani hapo mwaka 2011, dhidi ya DC Motema Pembe na kufungwa mabao 2-0 hivyo kuondolewa katika mashindano kwa jumla ya mabao 2-1.

Rekodi inaonyesha Simba haijawahi kushinda mechi yoyote katika ardhi ya DR Congo katika mechi zake tatu alizocheza nchini huo amefungwa jumla ya mabao 6-1.

Nchini DR Congo, Simba imefungwa bao 1-0 na AS Vita mwaka 1978, ikachapwa 2-0 na Motema Pembe 2011 kabla ya kunyukwa 3-1 mwaka huo na TP Mazembe jijini Lubumbashi.

Hii ni mara ya tatu kwa Simba na AS Vita kukutana kwenye mashindano ya Afrika.

Timu hizo zilikutana kwa mara kwanza katika hatua 8 bora ya mashindano ya CAF mwaka 1978. Vita ilifanikiwa kushinda kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kuifunga Simba hapa Dar es Salaam 1-0 na marudiano Kinshasa bao 1-0, hivyo historia inaonyesha Simba haijawahi kuifunga Vita katika mashindano yoyote.

Wakati Simba wakiwa na rekodi ya unyonge wapinzani wao AS Vita baada ya kufungwa 2-0 mechi ya kwanza na Al Ahly wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo wa nyumbani ili kurudisha matumaini yao katika Kundi D.

Katika kuhakikisha wanaondoka na ushindi Vita imepanga kuwatumia nyota wake wapya ambao hakucheza dhidi ya Al Ahly katika mchezo huo wa Jumamosi.

Pia, Vita wamewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Martyrs hapo Jumamosi kuishabikia timu yao.