VIDEO: Mkapa kuzikwa Julai 29 kijijini kwao

Muktasari:

Majaliwa amesema mwili wa Mzee Mkapa utaagwa kwa siku tatu kuanzia Julai 26-28, 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mzee Benjamin Mkapa atazikwa Julai 29, 2020 kijijini kwao Lupaso wilayani Masasi, Mtwara.

Majaliwa amesema mwili wa Mzee Mkapa utaagwa kwa siku tatu kuanzia Julai 26-28 katika Uwanja wa Uhuru ambapo, wananchi watapata fursa kwa siku zote hizo zote tatu.

Viongozi wa kiserikali, kidini na wageni kutoka mataifa mbalimbali wataaga hadi Jumanne ya Julai 28 kabla ya kusafirishwa kwenda kwao kwa maziko.

Awali, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ikimnukuu Rais John Magufuli imeeleza kuwa Rais mstaafu Mkapa alikuwa amelazwa jijini hapa.

Kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa tuendelee kumuombea mzee wetu ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito.

 

KUHUSU MZEE MKAPA

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 1938 wilayani Masasi mkoani Mtwara, ambapo aliiongoza nchi kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1995-2005.

Kiongozi huyo atakumbukwa kwa sera yake ya Uwazi na Ukweli na katika utumishi wake ikiwemo kusimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi. Aliweka mkazo katika ukusanyaji wa kodi ili kuwezesha Taifa kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendelea miradi mikubwa ya maendeleo.

 

Mwanaspoti kupitia mitandao yake ya kijamii itaendelea kukujuza kila kinachoendelea kwenye msiba huu mkubwa kwa Taifa. Pia, usikose kusoma gazeti la Mwanaspoti toleo la Julai 25, 2020 ambalo litakuwa na habari na Makala mbalimbali kuhusu Mzee Mkapa na utendaji wake hasa kwenye eneo la michezo.