VIDEO: Mashabiki waibana TFF ishu ya Morrison

Muktasari:

Baadhi ya mashabiki na wadau wa soka nchini wameendelea kufatilia sakata la Bernard Morrison dhidi ya waajiri wake Yanga kwa siku ya tatu ili kujua hatma.

MASHABIKI wa soka nchini wameendelea kujitokeza kwa wingi katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka kufahamu yaliyojiri katika sakata la mchezaji Benard Morrison.

Morrison yupo katika vuta ni kuvute baina yake na Yanga juu ya suala la kimkataba ambalo linaendelea katika kamati yaSheria na hadhi za wachezaji.

Mwanaspoti ambalo limeweka kambi katika ofisi hizo tangu saa 4:00 asubuhi, lilishuhudia mashabiki hao wakianza kufika saa 6:00 mchana.

Mashabiki hao walionekana kuwa na shahuku ya kutaka kufahamu nini ambacho kinaendelea lakini walijikuta wakikaa bila kujua hatma yoyote mpaka sasa.

Uwepo wa mashabiki hao kulifanya Polisi kuweka ulinzi wa kutosha ili kusiwe na vurugu yoyote ile na haikuweza kutokea.

Upande wa ulinzi kwa TFF unaosimamiwa na Suma Jkt wao walikuwa wamefunga geti na mtu anayetaka kuingia ndani ni lazima ujitambulishe kisha ndio unapewa nafasi ya kuingia.

 

MASHABIKI WAFUNGUKA

Shabiki anayefahamika kwa jina la Frank Yanga, alisema yeye yupo katika ofisi hizi kwa lengo la kuangalia namna nembo ya Yanga ikiwa salama.

"Unajua hapa nipo nikiangalia nembo ya Yanga na sio Morrison, kama kuna baya basi inachafuka nembo na sio mtu mimi wala sijali kuhusu Morrison kabisa, lakini viongozi kama vipi wamalize halafu yeye aondoke,"

Mdau mwingine aliyejitambulishwa kwa jina la Sekela alisema "Suala la Morrison litatuliwe kwa haki, kama Yanga wamekosea basi wapewe adhabu na kama mchezaji kakosea basi apewe adhabu hili suala liishe,"

Jana Mwenyekiti wa kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji, Elias Mwanjala alisema hatma ya mchezaji huyo itajulikana leo.