VIDEO: Mama 'ateka' mtoto kisa AS Vita

Muktasari:

Kivutio kikubwa ni dada, Ashura na mtoto wake Abdallah ambao wamevalia nguo zenye rangi zinazofanana na bendera ya nchi ya Congo na tayari wamewasili uwanjani muda huu.

Dar es Salaam. Vuguvugu la mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na AS Vita umeanza kupamba Moto baada ya mashabiki kuanza kuingia uwanjani mapema.


Licha ya mchezo huo kuanza saa 1:00 usiku, lakini mashabiki tayari wameanza kuingia jambo ambalo litawafanya kutumia masaa matano kukaa uwanjani wakisubiri mechi hiyo.

Kivutio kikubwa ni dada, Ashura na mtoto wake Abdallah ambao wamevalia nguo zenye rangi zinazofanana na bendera ya nchi ya Congo na tayari wamewasili uwanjani muda huu.

Dada huyu raia wa Congo amekuja uwanjani hapo kuishangilia AS Vita lakini cha kushangaza mtoto wake ni shabiki wa Simba na  anamkubali zaidi Mnyarwanda Meddie Kagere.

Ashura amesema amewahi kufika uwanjani mapema ili apate nafasi nzuri ya kukaa na nwanae na kuepuka vurugu kwani muda unavyosonga ndivyo mashabiki wanazidi kuwa wengi.

Mwanamke huyo ameitabiria AS Vita kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, mbele ya Simba wakati mtoto wake Abdallah akisema Simba itashinda.

"Mimi Ni Mcongo lakini naishi Tanzania na nimewahi uwanjani ili nipate sehemu nzuri ya kukaa na mwanangu hivyo hata kama mechi ni saa 1:00, usiku sioni kama ni mbali, Sitaki kabisa nipitwe na vitu vya hapa,"alisema Ashura.

"Mwanangu ni Simba kwa sababu baba yake ni shabiki wa Simba ila leo nimemteka lazima ashangilie AS Vita,"alisema Ashura.

Mtoto Abdallah alisema: "Mimi naishabikia Simba na nampenda Kagere".