VIDEO: Kimbunga Kagere chaikumba Al Ahly Taifa

Muktasari:

Bao hilo la Kagere sio tu limeifanya Simba ifikishe pointi sita kwenye msimamo wa kundi D la mashindano hayo bali pia limewafuta machozi mashabiki wa timu hiyo baada ya kupita kwenye nyakati ngumu katika mechi mbili zilizopita za mashindano hayo.

Dar es Salaam. Katika nyakati ngumu unahitaji shujaa mmoja atayekuweka mgongoni na kukuvusha kuelekea kule ambako unahitaji kufika.

Ndivyo unavyoweza kumuelezea mshambuliaji Meddie Kagere kwa namna alivyoweka hai matumaini ya Simba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Namna alivyofunga bao hilo ni darasa tosha kwa idadi kubwa ya washambuliaji wa hapa kutochezea nafasi ndani ya eneo la hatari la timu pinzani.

Akipokea vyema pasi ya kichwa kutoka kwa nahodha John Bocco, Kagere pasipo kutuliza alipiga shuti kali la mguu wa kulia ambalo lilimpita kwa kasi ya umeme, kipa mzoefu Mohamed El Shennawy na kutinga wavuni.

Bao hilo la Kagere sio tu limeifanya Simba ifikishe pointi sita kwenye msimamo wa kundi D la mashindano hayo bali pia limewafuta machozi mashabiki wa timu hiyo baada ya kupita kwenye nyakati ngumu katika mechi mbili zilizopita za mashindano hayo.

Kagere alifunga bao hilo pekee katika dakika 67, kwa shuti kali akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na John Bocco aliyepokea krosi kutoka kwa Zana Coulibaly.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Gor Mahia, Kagere amethibisha thamani yake mbele ya mashabiki wa Simba akiwa amefunga mechi zote za Ligi ya Mabingwa kuanzia hatua ya awali.

Katika mechi dhidi ya Mbabane Swallows mshambuliaji Kagere alifunga mabao mawili akifunga bao moja kila mchezo nyumbani na ugenini.

Kagere alifunga bao moja dhidi ya Nkana katika ushindi wa mabao 3-1 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hatua ya makundi Kagere alianza kwa kufunga mabao mawili dhidi ya JS Saoura katika ushindi 3-0 na leo amefunga bao lake la sita.

Idadi hiyo ya mabao inafanya Kagere kuongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na magoli sita akifuatiwa na Jean Marc Makusu wa AS Vita Club mwenye mabao 5.

Upande mwingine bao hilo lilikuwa ni kielelezo cha kiu ya Simba kuendeleza ubabe wake nyumbani katika mashindano hayo msimu huu.

Kwa Kagere bao hilo lilikuwa na maana kubwa kwake kwani mbali na kuipatia Simba pointi tatu muhimu pia limemfanya afikishe idadi ya mabao sita na kushika nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji nyuma ya Moataz Al-Mehdi wa Al Ahli Tripoli ya Libya mwenye mabao saba.

 Simba ilionyesha mabadiliko makubwa kwenye mchezo wa huo dhidi ya Al Ahly kulinganisha na mechi mbili kabla za hatua ya makundi ambazo waliruhusu jumla ya mabao 10, wakifungwa mabao 5-0 katika kila mechi.

Nidhamu ya hali ya juu waliyoonyesh kuanzia mwanzoni mwa kipindi cha kwanza hasa kwenye safu ya ulinzi pamoja na jitihada za mchezaji mmojammoja ndani ya uwanja, zilionyesha wazi kuwa Simba ilijifunza kutokana na makosa ya mechi zilizopita na iliyafanyia kazi.

Simba ambayo imekuwa ikisumbuliwa na mipira ya juu itokanayo na krosi, kona na faulo, wachezaji wake walihakikisha hawatoi nafasi kwa wapinzani wao kuwaadhibu nayo na tofauti na mechi zilizopita dhidi ya AS Vita na Al Ahly ugenini ambapo walifungwa mabao matatu ya namna hiyo.

Lakini leo walionekana kucheza kitimu pindi walipokuwa wakishambulia na hata pale mpira ulipokuwa kwa wapinzani wao, hawakutegeana kuusaka jambo lililowafanya watibue mipango ya Al Ahly mara kwa mara.

Haikushangaza kuona Simba ambayo ilionekana kuelemewa kwenye mchezo uliopita jijini Alexandria, Misri ikitakata na kufanya mashambulizi ya mara langoni mwa Ahly ambao walijaza idadi kubwa ya wachezaji eneo la katikati mwa uwanja.

Hata hivyo mipango mingi ya Simba kupenya safu ya ulinzi ya wapinzani wao, ilitibuliwa na viungo wawili wa ukabaji ambao Ahly iliwaanzisha kwenye mchezo wa jana ambao ni Hamdi Fathy na Amr Elsoulia.

Miongoni mwa nafasi ambazo Simba walishindwa kuzitumia kwenye mchezo wa leo ni nne ambazo walizipata kipindi cha kwanza ambazo zilipotezwa na Bocco, Cletous Chama, Okwi na Kagere katika dakika ya tisa, 12, 32 na ile ya 40.

Wakati Simba wakitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, Ahly walicheza soka la taratibu wakiwa kama wanawasoma Simba huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza ya hapa na pale.

Shambulizi kali ambalo Ahly walilifanya kwenye mchezo huo ni lile la kiungo mshambuliaji Karim Nedved ambaye aligongeana vyema pasi na Hassan El Shahat lakini shuti lake lilipiga nyavu za pembeni za Simba na kutoka nje.

Hata hivyo hadi kipyenga cha kuashiria kumalizika kwa dakika 45 za kwanza kilipopulizwa na mwamuzi Mahmood Ismail kutoka Somalia, timu hizo zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuendelea kumiliki  mpira na kulishambulia lango la Ahly ambao walionekana kama wameanza kuridhika na matokeo ya sare ambapo walianza mbinu za kupoteza muda hasa kipa na nahodha wao Mohamed El Shennawy.

Taswira ya mchezo huo ilikuja kubadilika mnamo dakika ya 64 baada ya Simba kupata bao hilo kupitia kwa Okwi ambaye hakufanya ajizi kutumia vyema pasi aliyotengewa na Bocco ndani ya eneo la hatari la Ahly na kupiga shuti lililojaa kimiani.

VIKOSI

Simba: Aishi Manula, Zana Coulibaly, Asante Kwasi/Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco/Muzamir Yassin, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.

Al Ahly: Mohamed Elshenawy, Karim Hassan, Yasser Ibrahim,Hamdy Fatah, Ayman Ashraf, Ramadan Ahmed, Hussein Elshanat, Amro Elsoulia, Ali Maaloul, Oliwafemi Ajayi na Mohammed Hany.