VIDEO: JK afunguka kauli ya mwisho ya Mzee Mkapa

Muktasari:

Kikwete amesema Mzee Mkapa hakuwa na ugonjwa wa kutisha ambao ungeweza kusababisha mauti yake

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye pia ni mdau mkubwa wa michezo hapa nchini, amesikitishwa na kifo cha Mzee Benjamin Mkapa.

Kikwete amesema Mzee Mkapa hakuwa na ugonjwa wa kutisha ambao ungeweza kusababisha mauti yake, lakini anamuachia Mungu kwa kuwa, wote wako njia moja.

Rais Kikwete, ambaye ni mdau mkubwa wa michezo aliyekabidhiwa Uwanja wa Taifa mwaka 2007 uliojengwa na utawala wa Mzee Mkapa, amesema jana Julai 23, 2020 alikwenda hospitali kumjulia hali na walizungumza mambo machache na kumuahidi kwenda kumjulia hali tena siku zijazo.

Akizungumzia kifo cha Mzee Mkapa wakati wa mahojiano na TBC, Kikwete amesema walizungumza na baadaye kuagana vizuri na Mzee Mkapa hivyo, kifo chake kimemshtua sana.

"Nilimwambia nitakuja kukuona kesho (leo Julai 24, 2020) ila sikuombei uendelee kukaa hospitali, natamani nije kukusalimia ukiwa nyumbani na yeye akaniambia: ‘nipo vizuri’.”

Kikwete ameongeza Taifa limepoteza moja ya viongozi mashuhuri ambaye, amelitunza Taifa kwa heshima kubwa na kwa moyo wa upendo hivyo, Watanzania waendelee kuomboleza, na kuwa na moyo wa subira.

Hata hivyo, Rais Kikwete amekumbusha kwamba, jambo la msingi ni kuyakumbuka mema aliyoyafanya na kuyapigania wakati wa uhai wake na kuendelee kuyaenzi.

Awali, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ikimnukuu Rais John Magufuli imeeleza kuwa Rais mstaafu Mkapa alikuwa amelazwa jijini hapa.

Kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa tuendelee kumuombea mzee wetu ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito.

 

KUHUSU MZEE MKAPA

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 1938 wilayani Masasi mkoani Mtwara, ambapo aliiongoza nchi kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1995-2005.

Kiongozi huyo atakumbukwa kwa sera yake ya Uwazi na Ukweli na katika utumishi wake ikiwemo kusimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi. Aliweka mkazo katika ukusanyaji wa kodi ili kuwezesha Taifa kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendelea miradi mikubwa ya maendeleo.

 

Mwanaspoti kupitia mitandao yake ya kijamii itaendelea kukujuza kila kinachoendelea kwenye msiba huu mkubwa kwa Taifa. Pia, usikose kusoma gazeti la Mwanaspoti toleo la Julai 25, 2020 ambalo litakuwa na habari na Makala mbalimbali kuhusu Mzee Mkapa na utendaji wake hasa kwenye eneo la michezo.