VIDEO: Chama mchezaji hatari zaidi Simba

Muktasari:

Chama alifunga mabao mawili na kutengeneza moja dhidi ya Biashara

Dar es Salaam. Kiungo raia wa Zambia, Clatous Chama amekuwa midomoni mwa mashabiki wa Simba na wapenda soka nchini kutokana na kiwango alichokionyesha juzi.

Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara United, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Chama alikuwa nyota kutokana na kufunga mabao mawili na kutoa pasi nzuri ya kisigino katika bao la nne.

Chama alifunga bao la kwanza akimalizia pasi ya Luis Luis Miquissone, akifanya hivyo pia katika bao la pili, huku mshambuliaji aliyepewa nafasi ya kuanza kwa mara nyingine, Meddie Kagere akifunga la tatu kabla ya pasi ya Chama kumpa nafasi Cris Mugalu kufunga la nne.

Miquissone alifanya makubwa kwa kutoa pasi tatu za mabao, lakini Chama aliteka mashabiki kutokana na aina ya mabao yake na kiwango chake kwa ujumla.

Kocha Sven alikuwa na mpango tofauti wa kuhakikisha anailazimisha Biashara kuwapa nafasi ya kucheza soka lao.

Mfumo wa 4-3-3 ulionekana kuwa bora kwa kila mchezaji wa Simba ndani ya uwanja, huku mikimbio ya Chama na Miquissone ikiwa na faida kutokana na uelewano wao.

Miquissone anaweza kuwa mchezaji bora wa mechi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujua kila aina ya mchezaji mwenzake uwanjani anataka mpira wa aina gani.

Utulivu wa wachezaji hao wawili ulikuwa na faida kubwa kwa miamba hiyo ya soka na kuwasahaulisha mashabiki wake kiwango kibovu katika michezo miwili iliyocheza dhidi ya Ihefu FC na Mtibwa Sugar na kuvuna alama nne.

Unaweza kusema kwa sasa, kama Simba inakuwa katika kiwango chake, Chama ndiye mchezaji hatari zaidi wa kumwangalia kutokana na kuwa na kazi zaidi ya moja uwanjani.

Kocha wa zamani wa Prisons, Mohammed Adolph Rishard, alisema Simba ilicheza vizuri huku akikiri Chama ni mchezaji mwenye akili ya soka na akimsifu Miquissone kuwa na kipaji na kasi.

“Walicheza kwa kiwango bora sana na hata muunganiko wa Chama na Miquissone ulikuwa mzuri kutokana pia na uwanja waliocheza.

“Uwanja wa Taifa unahamasisha wachezaji kucheza mpira mzuri kwani hata timu za mikoani zinapokuja kwenye uwanja kama huko zinafurahia kucheza pale na ndiyo maana uliona wachezaji kama Chama, Miquissone walikuwa katika ubora wao,”alisema Rishard.

Kocha Mrage Kabange alisema Miquissone na Chama ni wachezaji wazuri lakini walikuwa bora zaidi juzi na kuchangia kwa kisia kikubwa ushindi wa timu yao.

“Wote walicheza pamoja katika mechi ya Mtibwa, lakini uwanja haukuwa rafiki kwao na ndiyo maana nasema ni lazima wapambane hata katika viwanja kama vile.

Katika mechi za jana, KMC ilirudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Laurient Lusajo dhidi ya Mwadui FC, kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, mkoani Shinyanga.