VAR yaleta utata kulikataa bao la Samatta akiifunga Liverpool

Muktasari:

 KRC Genk watacheza tena na Liverpool katika mchezo ujao wa Ligi bya Mabingwa Ulaya  lakini safari hii itakuwa ugenini  kwenye uwanja wa Anfield.

Dar es Salaam. Teknolojia ya usaidizi wa video  kwa waamuzi 'VAR', imezima ndoto ya nahodha wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta  kuifunga Liverpool kwenye mchezo wa jana wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakati Liverpool wakiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Oxlade-Chamberlain, Samatta alifunga bao, ambalo lingekuwa la kusawazisha kwa kichwa katika kipindi hicho cha kwanza, lakini mwamuzi wa mchezo huo,Slavko Vincic  aliomba usaidizi wa VAR.

Baada ya kutazamwa bao lile la Samatta, Mslovenia ambaye alikuwa akichezesha mchezo huo, alilikataa huku wengine wakidhani kuwa kumtuia kwake James Milner kama ngazi ilichangia na wengine wakiliona tukio lile kuwa huenda alikuwa kwenye eneo la kuotea.

Hivyo hadi mapumziko, KRC Genk walienda kupumzika wakiwa nyumba kwa bao 1-0, mambo yaliwaendea kombo katika kipindi cha pili kwa kuongezwa mengine matatu licha ya kupata moja la kufutia machozi kupitia kwa Odey.

Mabao mengine ya Liverpool kwenye mchezo huo, yalifungwa na Oxlade-Chamberlain kwa mara nyingine tena huku, Sadio Mane na Mohammed Salah kila mmoja akifunga bao moja.

KRC Genk: Coucke, Mæhle, Cuesta, Lucumi, Uronen, Ito (87 'Hagi), Berge, Heynen, Bongonda (67' Ndongala), Samatta na  Onuachu (81 'Odey).

Liverpool FC: Alisson, Fabinho, van Dijk, Lovren, Milner, Keïta, Firmino (80 'Origi), Mané, Salah, Oxlade-Chamberlain (74' Wijnaldum) na  Robertson (64 'Gomez).