Uzalendo ulioonekana pambano la watani uhamie Stars

Friday October 5 2018

 

Ukimwona kobe ametulia yakupasa ujue anatunga sheria. Kwa sasa, sio mitaani, vitongojini, vijijini, wailayani, mikoani hadi Taifa pametulia tuli. Ndio, hakuna tena kelele, baada ya kile kipindi kisichozidi siku kumi kupita.

Ni kipindi kilichotawaliwa na kila aina ya tambo, kejeli, vijembe na masihara mengi wakati mashabiki na wapenzi wa soka hasa wa timu hizi kongwe Simba na Yanga walipokuwa wakilisubiri kwa hamu pambano hilo la watani wa jadi lililopigwa Jumapili iliyopita.

Wote wanatokea mitaa ya Kariakoo, mmoja akitokea mitaa ya Msimbazi na mwingine Jangwani katikati kabisa ya Jiji la Dar es Salaam.

Hadi septemba 20, zote zilikuwa zimemaliza mechi zao mwisho kabla ya wao wenyewe kukutana hiyo Jumapili iliyopita. Yanga ilitoka

Kumfunga Singida United mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, huku Simba ikiizima Mwadui FC kule kwao Shinyanga kwa mabao 3-1. Baada ya hapo, akili za wapenzi wa soka zikahamia kwenye mpambano huo wa watani wa jadi.

 

Si rahisi kupima ukubwa na kiwango cha vugu vugu au jotoridi (temperature) ya mechi baina ya timu hizi zinapokutana, isipokuwa huwa kuna viashiria vingi mbali mbali vinavyoonesha dalili za kwamba ndani ya mipaka ya nchi yetu na hata nje ya mipaka, pambano hili linavuta hisia za watu wengi na huu umekuwa ni utamaduni wa mchezo huu.

Zipo derby nyingine hapa nchini kama vile Mbeya City dhidi ya Prisons n.k lakini hii ya watani wa Kariakoo ni ya aina yake,siyo tu hapa Tanzania lakini pia barani Afrika.

Utulivu huu tunaouona leo hii ni baada tambo na vitimbwi vyote kutoka pande zote mbili kuhitimishwa na filimbi ya mwanamama mahiri  Jonesia Lukyaa Kabakama aliyekabidhiwa jukumu la kusimamia na kuzitafsiri sheria zote kumi na saba zinazotawala mchezo wa soka katika kila dakika tisini za mchezo.Ama kwa hakika katika pambano hili mwamuzi huyu mwenye beji ya Fifa alivyosimama imara na kuitendea haki kazi yake na hadhi yake akiwa ni mwamuzi wa ligi kuu (TPL),kwa wale wote tulioshuhudia mchezo ule tumeona ni kwa nini shirikisho la soka duniani Fifa limemteua kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha michuano mikubwa ya wanawake duniani. 

Katika hali ya kawaida binadamu tuna hulka ya kurahisisha majukumu ya watu hasa pale tunapokuwa tunatazama ama kuangalia kazi ya mwingine mwenye wajibu wa moja kwa moja katika kutekeleza jukumu fulani, mathalani wakati mchezo unapokuwa unaendelea kiwanjani tumezoea kusikia kutoka kwa watazamaji walioketi majukwaani wakitoa maoni au wakati mwingine kuwalaumu wachezaji au waamuzi katika matukio mbali mbali “ ahaaaa…….kakosa bao la wazi kabisa si angepiga kule au pale….? Lakini wanasahau kwamba kuna mambo mengi yanayoweza kujitokeza kiasi cha kumfanya mshambuliaji apoteze nafasi. Vivyo hivyo kwa mwamuzi wa mpira mambo siyo mepesi sana kama wengi tunavyofikiri,pale katikati ya kiwanja pagumu na hasa kwenye mechi ngumu kama ile ya Yanga na Simba. Kama nchi kupitia shirikisho la soka Tanzania tunahitaji kuendelea kuwaibua na kuwaandaa waamuzi wengi wenye viwango vizuri wa jinsia zote , hiyo itakuwa ni hatua mojawapo nzuri ya kuleta maendeleo ya mchezo huu hapa nyumbani .

Mechi ya watani wa jadi imetuonesha mambo mengi kama ilivyo desturi timu hizi zinapokutana.Mara nyingi kila baada ya pambano kukamilika iwe ni kwa timu moja kushinda ama sare yatazungumzwa au kusemwa mengi,na kila mmoja akiamini kwamba yupo sahihi na kama anakosea ni mara chache kukiri kwamba anakosea,na hapo ndipo msingi wa ubishi na malumbano mengi ulipo.Katika hali ya kawaida vuguvugu la mazuri na mabaya hoja zake zinapatikana zikiwa na maana au kupoteza maana.

Licha ya yote hayo mechi ya mwishoni mwa juma lililopita (Simba vs Yanga) iliwapa burudani wapenzi na mashabiki wa soka kwa kiwango kilichotarajiwa kutokana na jinsi vikosi vya timu zote vilivyokuwa.Kwa ujumla wachezaji walikuwa wameandaliwa kikamilifu kwa ajili ya mbinu na ufundi ambao ungesaidia kuzipa matokeo mazuri.Baada ya dakika tisini za mchezo kilichotokea kilitafsiri kushinda au kushindwa kwa matumizi ya mbinu zilizotumika.Kwa watazamaji,wapenzi na mashabiki hawana nafasi kubwa ya kulisemea hilo  kwani malengo ya mbinu hizo yanajulikana zaidi kwa walimu na benchi zima la ufundi.

Sambamba na hilo wachezaji kwa upande wao walijitahidi sana kila mmoja katika nafasi yake na uwezo wake kutuonesha ufundi wao kutegemeana na vipaji walivyonavyo na mwisho wa siku tulishuhudia muunganiko wa stadi za kucheza soka ambao uliainisha ubora wa kila upande kama timu.Kwa ujumla mchezo ulikuwa na sura mbili, moja ni timu kushambulia kwa muda wote wa mchezo na mbili ni timu kujilinda kwa muda wote.Pamoja na mchezo kuwa na sura mbili za mbinu mahususi (kujilinda na kushambulia), wachezaji wa timu zote mbili kwa asilimia tisini ( 90% ) walicheza kwa kujituma na kujitolea mno ili kuzipatia timu zao matokeo chanya hali iliyotafsiri moyo wa uzalendo wa hali ya juu wa kuzipigania timu zao,tunawapongeza kwa kutuonyesha tabia hiyo.

Sote tunafahamu kwamba wakati huu ratiba ya Caf ya michuano ya kuwania kufuzu fainali za Afcon inaendelea na tayari timu yetu ya taifa ipo kwenye kampeini ya kutafuta nafasi hiyo ambayo watanzania wote tungetamani kuipata ukizingatia kwamba ni muda mrefu sana hatujaweza kufanya hivyo tangu enzi za kina Tenga na wenzake mwaka 1980.

Hakika ni mbali sana, hivyo jeshi letu la sasa linaloongozwa na nahodha Mbwana Ally Samatta, linahitaji kujiuliza,kujitolea lakini zaidi ya yote kutambua kwa kiwango cha juu sana kiu ya wananchi na matarajio yetu kwa hawa wachezaji walioitwa kwenye timu ya taifa.

Maswali ni mengi na yataendelea kuongezeka hadi hapo yatakapopatikana majibu tunayoyataka. Swali kubwa kuliko yote ni je? kushindwa kwa timu yetu kucheza fainali kwa muda mrefu kiasi hiki kunasababishwa na nini?, imekuwa vigumu sana kupata majawabu ya mwisho,lakini juhudi  za hapa na pale zikiwa zinaendelea kufanyika.Katika mchakato wa kutafuta sababu ,mengi yamekuwa yanatajwa lakini wakati fulani katika nyakati tofauti kumetokea hoja za kwamba baadhi ya wachezaji wetu wanaopata bahati ya kuitwa kwenye timu ya taifa huwa hawana moyo na mapenzi makubwa ya kuitumikia timu yao ya taifa. Hili linaweza kuwa ni tatizo miongoni mwa yale yanayotukwaza.

Ujenzi wa timu yoyote unahitaji yafanyike mambo mengi kwa ajili ya kuwa na wachezaji wa kupata ushindi ambayo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu, ufundi, mbinu na saikolojia. Ni kwa msingi huu kila kukicha shirikisho la mpira Tanzania linajaribu kutafuta wataalamu wa kufanikisha  eneo hili.

Mpaka sasa katika kundi letu la L tunaonekana ni washindani kwani katika michezo miwili tuliyocheza tuna alama mbili dhidi ya Lesotho na Uganda,baada ya kutoka sare michezo yote, kwa muda usiozidi wiki mbili zijazo tutacheza na Cape Verde ugenini na nyumbani, mchezo wa kwanza utakuwa huko kwao tarehe 13/10 na mchezo wa marudiano utakuwa hapa nyumbani tarehe 16/10 ina maana ndani ya siku nne (4) michezo yote miwili. Siyo michezo rahisi ukizingatia nafasi ya wenzetu kwa maana ya viwango vya ubora wa soka duniani, sisi tukiwa nafasi ya mia moja na arobaini (140), wao wapo juu yetu kwa mbali katika nafasi ya sitini na saba ( 67 ), kwa takwimu zilizotolewa mwezi September tarehe 20.

Siyo wote waliopo kwenye timu ya taifa walicheza mechi ya Simba na Yanga, tuna hakika kwa upambanaji wa kiwango kile lazima Cape Verde atafungwa, tunasubiri kwa hamu tuwaone wakihamishia nguvu na moyo wa kujituma na kujitolea kwa ajili ya taifa lao.

Advertisement