Uwanja wa Simba SC wawapa dili Mamalishe, Bodaboda

Muktasari:

Wafanyabiashara wadogo wadogo walioanza kula matunda ya uwepo wa uwanja huo ni mama lishe na madereva bodaboda.

Dar es Salaam.Wafanyabiashara wadogo wadogo wameanza kunufaika mapema na uwepo wa Uwanja wa Simba kwa kuuza biashara zao kwa watu mbalimbali wanaokwenda kuangalia ujenzi wa uwanja huo uliopo Bunju.

Wafanyabiashara wadogo wadogo walioanza kula matunda ya uwepo wa uwanja huo ni mama lishe na madereva bodaboda.

Mama lishe aliyejitambulisha kwa jina la Tausi alisema kuwekwa nyasi bandia uwanja huo wananufaika kibiashara kutokana na idadi kubwa ya watu wanaokwenda kuutazama.

"Awali nilikuwa siwezi kuuza kumaliza chai, maandazi na kashata, lakini kwa sasa nauza sana mfano leo hii ni mara ya tatu kupika hadi nachoka,"alisema Tausi.

Naye dreva bodaboda, Deo Kalia alisema hawajaishia kupiga pesa kutokana na watu wanaokwenda kutazama nyasi bandia zilizoanza kutandikwa.

Amesema kabla ya kuanza ukarabati huo kulikuwa hakuna umeme na maji safi, lakini kwa sasa wanapata huduma hizo.

"Mwanzo tulikuwa tunakunywa maji ya kwenye makorongo, lakini sasa tunakunywa maji masafi, umeme tunaweza kuchukulia hapo kuweka majumbani mwetu,"

"Kijiwe changu mwanzo kilikuwa kule juu sasa hivi nafanyia hapa jirani na uwanja kwa sababu wateja wapo wengi, maendeleo yameanza kuja, tunawashukuru Simba," alisema Kalia.