Uwanja wa Nangwanda Sijaona wafungwa kupisha ukarabati

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi mkoani Mtwara kimefunga uwanja wake wa Nangwanda Sijaona kwa muda ili kuufanya ukarabati kuweza kuendana na mahitaji ikiwa ni pamoja na kuboresha vyoo.

Mtwara. Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara kimeufunga kwa muda Uwanja wa Nangwanda Sijaona unaomilikiwa na chama hicho ili kufanyiwa ukarabati kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Uwanja huo umekuwa ukitumiwa na Ndanda FC inayoshiriki Ligi Kuu pia wiki iliyopita ulitumika kufanyia  mashindano mbalimbali ikiwemo Umiseta na Umitashumta.

Akizungumza katibu wa CCM Mtwara, Alhaj Saad Kusilawe Kasilawe amesema kwa sasa hawaruhusu kufanyika kwa shughuli yoyote kwenye uwanja huo kutokana na kuwepo kwa mapungufu ikiwemo kurekebisha pitch na kuhakikisha nyasi zinamwagiwa maji ya kutosha ili kukuwa na kuendana na mahitaji ya mchezo sambamba na kurekebisha vyoo vyote vinavyohitajika uwanjani hapo.

“Baadhi ya maeneo kuna mapungufu ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho, sasa ratiba ilivyo ni kwamba mwezi ujao ligi itanza tukaona si vyema tukachelewa, kwa hiyo tumeamua kwa makusudi kuanzia leo tnaufunga usitumike kwa michezo ya aina yoyote ili tufanye kazi ya kuukarabati,”amesema Kusilawe

 Mmoja wa wakazi wa Mtwara, Severine Mkumi amesema uamuzi hayo ni muhimu kuukarabati uwanja ili wachezaji waweze kucheza katika uwanja uliokidhi mahitaji.

Mkazi mwingine Waziri Said alisema “Wakati wanaangalia uwanja ni vyema wakaboresha na majukwaa ili mashabiki waweze kuangalia mpira kwa utulivu kwani mpira ni sehemu ya burudani, mazingira yanapokuwa mazuri mashabiki nao wataongezeka.”