Uvivu wetu ndio unaotuumbua

Muktasari:

  • Lakini ni kama Ofisa wa CAF, Gaye hakupaswa kutoa kauli kama ile kwa sababu alitakiwa awe wa kwanza kujua kimahesabu kuwa Tanzania ilikuwa haijatolewa.

KAMA taifa waandaaji, wamekuwa timu ya kwanza kuyaaga mashindano.

Hii ilikuwa kauli ya Ofisa Habari wa CAF, Mamadou Gaye kwa Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo wa Tanzania na Uganda, Aprili 17, 2019.

Kauli hii ilikuja baada kipigo cha 3-0 ambacho timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya miaka 17 ilikipata kutoka kwa wenzao wa Uganda.

Kipigo hicho kilichokuwa cha pili baada ya kile cha 5-4 kutoka Nigeria, kilionekana kuhatarisha ndoto ya Tanzania kufuzu Kombe la Dunia U-17 kwa mwaka huu zitakazofanyika Brazil.

Lakini ni kama Ofisa wa CAF, Gaye hakupaswa kutoa kauli kama ile kwa sababu alitakiwa awe wa kwanza kujua kimahesabu kuwa Tanzania ilikuwa haijatolewa.

Kauli yake ingeweza kutafsiriwa kama kauli rasmi ya CAF na kuleta mkanganyiko mkubwa.

Zaidi ya kuwa Ofisa wa CAF, Gaye amekuwa mchambuzi wa soka la Afrika kwa muda mrefu, tangu akiwa Super Sport sambamba na mwenzake Thomas Mlambo.

Kwa sifa hiyo, alipaswa kufanya hesabu zake mapema na kuwasaidia watu kuelewa kuliko kuwapotosha, kama alivyofanya.

Ni bahati nzuri kwamba Mirambo mwenyewe alikuwa akijua kwamba nafasi bado ipo...japo kimahesabu!

Hata hivyo, licha ya Mirambo kueleza kwamba kimahesabu nafasi bado ilikiwepo, waandishi wa Tanzania waliopata nafasi ya kuuliza maswali, waliendelea kusisitiza kwamba nafasi haipo, wengine wakitumia kigezo cha mechi za ana kwa ana dhidi ya Uganda.

“Hata kama Tanzania itaifunga Angola, itakuwa imetolewa kwa sababu ilifungwa na Uganda,” alisema mwandishi mmoja.

Kimsingi Mamadou Gaye na waandishi wengine wa Tanzania waliopata nafasi ya kuuliza, waliitumia kibubusa zaidi ya kiuweledi.

Mwandishi au mchambuzi hapaswi kuwa na uelewa mdogo kama shabiki wa kawaida. Hapaswi kufuata mkondo bila kuwa na ujuzi nao....hapa ndipo neno kibubusa linakuja, yaani kutojifikirisha katika jambo zaidi ya kukubali kupelekeshwa tu.

Kuna tofauti kubwa ya shabiki wa kawaida na mwandishi wa habari au mchambuzi.

Shabiki wa kawaida hana muda wa kufuatilia mambo kwa kina na kiufundi. Hata kama atakuwa nao, lakini anaweza kukosa nafasi ya kufika sehemu husika kupata taarifa sahihi.

Shabiki wa kawaida hawezi kwenda TFF kuomba na akapewa hata kanuni za mashindano ya daraja la nne. Lakini mwandishi au mchambuzi anaweza kuomba na kupewa.

Tofauti hii ndiyo husababisha shabiki asiye makini aendeshwe kibubuswa kwani anakuwa hana hili wala lile katika jambo analoshabikia ila hufuata upepo tu na mwandishi awe kama mjuzi.

Atakachoandika mwandishi au atakachochambua mchambuzi, ndicho atakachokipata ndugu shabiki.

Lakini waandishi na wachambuzi wetu hawataki kuitumia nafasi hiyo na wao wameamua kufanya kazi kibubusa tu, yaani kuongozwa na hisia badala ya weledi na ujuzi wa mambo.

Kimsingi, baada ya kipigo cha 3-0 kutoka Uganda, Tanzania ilijiweka katika nafasi mbaya kwenye msimamo, lakini haikuwa na maana kwamba imeshatolewa moja kwa moja.

Sura ya 7 ibara ya 13.3 (c) inayosimamia mashindano yote ya CAF, yakiwemo haya ya vijana (kifungu kidogo cha pili) inasema kwamba ENDAPO TIMU ZAIDI YA MBILI ZITALINGANA POINTI, TOFAUTI YA MABAO YA KUFUNGA NA KUFUNGWA ILIYOPATIKANA KWENYE MECHI BAINA YAO WENYEWE, itatumika.

Lakini kutokana na uvivu wa kuzisoma kanuni na taratibu za mashindano, wengi walishindwa kuelewa na kujikuta wakileta mkanganyiko.

Mkanganyiko huu ni sawa na ule uliotokea mwaka 1998 pale Yanga ilipofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Magazeti mengi ya wakati ule yakiandika kwamba Yanga imefuzu robo fainali. Na hii ni kwa sababu waandishi wa wakati ule hawakujishughulisha kuyajua vizuri mashindano waliyoyaripoti ambayo yalianza mwaka mmoja kabla. Mwaka 1997, CAF ilibadilisha mfumo na muundo wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, yaliyoanza 1964 kuingia kwenye mfumo huu wa sasa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mfumo na muundo wa zamani uliyaendesha mashindano hayo kwa mtoano kuanzia mwanzo hadi mwisho. Muundo na mfumo mpya ukaleta hatua ya makundi ambapo zile timu ambazo zamani zilifuzu kwa robo fainali, kuanzia 1997 ziliingia hatua ya makundi.

Lakini waandishi wetu wa wakati huo (pamoja na kazi nzuri waliyoifanya) walishindwa kujua muundo na mfumo mpya, wakabaki na ule wa zamani.

Ndiyo maana badala ya kuripoti mashindano yale kwa jina jipya la Ligi ya Mabingwa, wao waliendelea kuyaita Klabu Bingwa. Mkanganyiko ule ulienda mbali zaidi hadi kufika ikulu ya soka pale Karume. Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, alisema kwamba Yanga imetinga nusu fainali.

Rage ni kama hakuwa akiufahamu sawasawa mfumo mpya ambao wakati ule ulizipeleka moja kwa moja timu kwenye fainali timu zilizoongoza makundi yao.

Kwa kuwa kawaida huendi fainali kabla ya nusu fainali, lakini Rage pengine furaha ilimzidi kwa timu ya Tanzania kufuzu hatua hiyo kwa mara ya kwanza naye akasahau na kusema Yanga walifuzu nusu fainali.

Tatizo lingine lipo kwa waandishi wetu.

Ukweli wengi ni wavivu wa kusoma. Kiukweli, uvivu ni kitu kibaya sana. Mara kadhaa kuendekeza kwetu uvivu kumekuwa kukituumbua kama waandishi na wachambuzi wasiotaka kushughulisha akili zao wanavyoumbuka mara kadhaa hadharani. Halafu kama hujui, hili Neno uvivu ni baya sana, ndio maana hata ukianza kulisoma kuanzia kulia, bado linasomeka hivyo hivyo...UVIVU!