Uturuki yaiduwaza Sweden nyumbani

Muktasari:

  • Sweden jana iliikaribisha Uturuki katika mchezo wa pili wa mashindano Euro Nations League, uliochezwa mjini Solna na ikafanikiwa kuongoza kwa mabao 2-1 hadi dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika lakini mabao mawili ndani ya dakika nne za mwisho yaliyofungwa na Emre Akbaba yakawaliza wenyeji.

Solna, Sweden. Kocha wa timu ya Taifa ya Sweden, Janne Andersson, 55, hajui imekuwaje na amlaumu nani kufuatia vijana wake kuzembea na kuwaruhusu Uturuki kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuibuka na ushindi katika dakika za lala salama.

Sweden jana iliikaribisha Uturuki katika mchezo wa pili wa mashindano Euro Nations League, uliochezwa mjini Solna na ikafanikiwa kuongoza kwa mabao 2-1 hadi dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika lakini mabao mawili ndani ya dakika nne za mwisho yaliyofungwa na Emre Akbaba yakawaliza wenyeji.

Katika mchezo huo Sweden walienda mapumziko wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Isaac Thelin katika dakika ya 34 na Claesson akaongeza la pili katika dakika ya nne ya kipindi cha pili hivyo kuongoza kwa mabao 2-0.

Hata hivyo vijana wa Uturuki waliocheza mpira mwingi walijipatia bao la kwanza katika dakika ya 51 likifungwa na Hakan Calhanoglu kabla ya Akbaba kufunga la kusawazisha dakika ya 88 na katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza akafunga la ushindi.

Ni mabao hayo ya Akbaba yaliyomfanya Kocha wa Sweden kukosa wa kumnyooshea kidole badala yake akasema timu nzima itabeba lawama katika hilo iwapo watashindwa kutinga hatua ya pili ya Nations League.

“Siwezi kumnyooshea mchezaji mmoja kidole lakini katika hili timu nzima inawajibika tumefanya uzembe usiokubalika katika soka, nadhani vijana wa Swedes, walilewa matokeo kabla ya mwamuzi kuhitimisha mchezo na hili ni kosa kubwa,” alisema.

Vijana hao wa Kocha Andersson, kwa sasa ndio wanaoburuza mkia kwenye kundi lao na wataifuata Russia katika mchezo ujao wa mashindano hayo utakaopigwa Oktoba 11 mjini Kaliningrad.