Utata waibuka umri Afcon

Muktasari:

  • Pamoja na kipimo hicho cha MRI kuwapitisha, maumbile ya baadhi ya wachezaji yameonekana kuleta hisia kuwa wana umri mkubwa kuzidi ule halisi wa chini ya miaka 17.

Dar es Salaam. Wakati fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana (Afcon) yakiendelea nchini, suala la umri wa wachezaji wanaoshiriki michuano hiyo limeibua utata.

Licha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumia vipimo vya MRI, ili kuthibitisha umri wa wachezaji kwenye Fainali za Afrika (AFCON U17), wasiwasi wa kutumika kwa wachezaji waliozidi umri kwenye mashindano hayo umeibuka.

Pamoja na kipimo hicho cha MRI kuwapitisha, maumbile ya baadhi ya wachezaji yameonekana kuleta hisia kuwa wana umri mkubwa kuzidi ule halisi wa chini ya miaka 17.

Hilo limepelekea baadhi ya makocha wa timu zinazoshiriki mashindano hayo kuonyesha wasiwasi kuwa huenda kipimo hicho sio suluhisho sahihi la kudhibiti upandikizaji wa vijeba mashindanoni.

“Unapata shaka na vipimo, lakini kuna wakati unakuwa hauna jinsi. Kama inafikia hatua wachezaji wawili mapacha ambao wamezaliwa wakati mmoja, kipimo kinaonyesha kuwa mmoja ana umri mkubwa na mwingine ana umri mdogo, inaleta wasiwasi,” aliseka kocha Oscar Mirambo.

Kocha wa Morocco, Pedro Goncalves licha ya kutonyooshea kidole moja kwa moja katika suala la umri, alitoa kauli inayoonyesha wasiwasi wa uwepo wa wachezaji wenye umri mkubwa.

“Mashindano haya ni mazuri kwa sababu yana kundi kubwa la wachezaji waliopevuka kulinganisha na mashindano mengine ya vijana wa umri kama huu,” alisema Goncalves.

Naye kocha wa Cameroon, Thomas Libih alisema kuwa kipimo cha MRI kimekuwa kikitoa majibu ya kushangaza jambo ambalo linatia shaka.

Kabla ya kuanza kwa fainali za Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 zinazofanyika hapa nchini, wachezaji sita wa timu tofauti walienguliwa kwenye vikosi vyao kutokana na kuonekana wana umri mkubwa zaidi ya miaka 17.