Utamwambia nini Mwanahamisi kuhusu Okwi

Muktasari:

Alisema amebaini kwa nini Okwi ufalme wake Simba unadumu licha ya kufifia na kurejea upya kutokana na uwepo wa Meddie Kagere ambaye anaonekana kuwateka mashabiki kutokana na uwezo wake.

MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Mwanahamisi Omary, humwambii kitu kuhusu Mganda Emmanuel Okwi wa timu ya wanaume namna anavyompenda kinomanoma.

Amefichua Okwi ni mchezaji pekee anayevutiwa na maujuzi yake ya uwanjani, akidai hana papara za kukera zaidi ya kuwapa raha mashabiki wake kwa namna anavyolijua goli, nidhamu na akili ya mpira.

Alisema amebaini kwa nini Okwi ufalme wake Simba unadumu licha ya kufifia na kurejea upya kutokana na uwepo wa Meddie Kagere ambaye anaonekana kuwateka mashabiki kutokana na uwezo wake.

“Kama kuna mwanasoka wa kiume ambaye natamani kuwa kama yeye kikazi ni Okwi, napenda kujifunza vitu vingi kutoka kwake ingawa siwezi kufikia mafanikio yake kwani soka la wanawake halilipi kama ilivyo kwa wanaume.

“Pamoja na msimu huu anaonekana kwake una changamoto nyingi haziwezi kuondoa ukweli Okwi anajua, naangalia vitu vingi kiufundi na Okwi sio kama wachezaji ambao wanakuja moto mwisho wake unakuwa ovyo,” alisema.

CHANGAMOTO

Achana na stori za Mwanahamisi, Kocha wa kikosi hicho, Omary Mbweze alikiri kitendo cha timu hiyo kuweka kambi Buguruni ambako hakuna utulivu ni changamoto kwao, ingawa alidai anaamini wachezaji wanajielewa hivyo watajitunza. “Ukweli, tumejitahidi kuweka ulinzi ili wasije wakaingia kwenye vishawishi ingawa naamini wanajielewa wapo kwenye timu kwa ajili ya nini,” alisema.