Utamu wa Yanga mpya uko hapa

YANGA jana ilitua Bukoba mapema tu ikiwa ni saa chache tangu itoke kutoa shoo safi pale Chamazi Complex na kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mlandege kwenye mechi ya kirafiki. Katika mechi ambazo Yanga imecheza hadi sasa kuna mambo ya kiufundi yameonekana kwenye kikosi chao kipya.

Kwa vyovyote Kocha Zlatko Krmpotic ni kama ameshapata kikosi cha kwanza ambacho kwa wafuatiliaji wa soka watabaini kilianza dhidi ya Mbeya City na badae kikaingia kipindi cha pili na Mlandege licha ya kwamba kilikuwa na mabadiliko kidogo sana.

Kwa mujibu wa mazoezi ya Kocha huyo pamoja na mtiririko wake langoni atamsimamisha, Faroukh Shikhalo, kwenye ukuta Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto na Kibwana Shomary Kibwana wakati kati atakuwemo Mukoko Tonombe na Feisal Salum. Watakaomaliza ni Deus Kaseke, Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne na Michael Sarpong.

Ingawa kwenye mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya Kagera huenda kisionekane kikosi hicho kamili kutokana na majeruhi waliobaki Dar es Salaam akiwemo kipa Shikhalo. Kiufundi katika kikosi kipya cha Yanga utamu ni mabadiliko ya soka la kocha huyo kama ifuatavyo;

KUKABA KUANZIA JUU

Katika mechi tatu ambazo Yanga imeshacheza mpaka sasa chini ya Krmpotic zikiwa mbili za ligi na moja ya kirafiki ya juzi usiku dhidi ya Mlandege na kushinda mabao 2-0, Yanga imeonekana kubadilika ambapo jukumu la kukaba linaanzia kule mbele.

Kocha huyo raia wa Serbia amekuwa mkali akitaka kuona kila mchezaji anakuwa na jukumu la kutafuta mpira pale tu unapopotea na kuwa katika himaya ya wapinzani.

HATAKI ANAOANAO

Ugomvi mkubwa wa Krmpotic na baadhi ya wachezaji wake ni kwamba hataki mtu anayekaa na mpira kwa muda mrefu na hilo alionyesha zaidi juzi akiwa mkali kwa kiungo Abdulaziz Makame ambaye alikuwa akitaka kukaa sana na mpira. Tathmini ya kiufundi inaonyesha kwamba ni Kocha anayetaka timu iwe bize muda wote si mtu mmoja.

PASI ZA KWENDA MBELE

Ugomvi wake mkubwa mwingine na Makame ukawa hataki kuona anapiga sana pasi za kulia na kushoto wala kurudisha mpira kwa mabeki bila sababu na kutaka kuona pasi anazotaka ni zile za kwenda mbele kutengeneza mashambulizi.

Kuanzia mazoezini anataka kuona timu ikipanda kwa kasi kwa kupitia aina hiyo ya uchezaji kwavile anao wachezaji wenye uwezo huo.

MASHUTI

Ubora mwingine wa soka la Krmpotic ni kwamba amewabadilisha wachezaji wake kupiga mashuti makali wanapokaribia katika lango la wapinzani na sasa yanapigwa mengi.Faida kubwa ya ubora huo ndio ukazalisha bao bora la kiungo mkabaji Mukoko Tonombe akifunga kwa shuti kali bao la pili la timu hiyo katika ushindi wa juzi wa mabao 2-0 dhidi ya Mlandege ya Zanzibar.

Mbali na shuti hilo la Tonombe pia ubora huo ulionekana kwa mshambuliaji Yacouba Sogne, beki wa kulia Kibwana Shomari, Feisal Salum, winga Tuisila Kisinda na Carlinhos. Wamekuwa watu wa mashuti makali nay a mbali ambayo yamekuwa pia burudani kwa mashabiki.

MABEKI WA PEMBENI

Kazi kubwa ya mabeki wa pembeni ni kukaba lakini wanapopandisha mashambulizi akili yao inatakiwa kuwa moja tu kupiga krosi zenye faida na sio ilimradi krosi.

Hapa Krmpotic amekuwa mkali kwa mabeki wake wa kushoto na mambo yamekuwa na nafuu kwa Kibwana Shomari na Yassin Mustapa ambao angalau wamekuwa wakikaribia kutimiza anachotaka kocha huyo.

TONOMBE AFUNGUKA

Akizungumza na Mwanaspoti Tonombe alisema kocha wao anataka kuona viungo wanakuwa na akili ya kutengeneza mashambulizi ya haraka kwa pasi zao za kwenda mbele na zinazofika.

Tonombe alisema ukiwa na ubora wa kupiga pasi ndefu au hata fupi lakini za kwenda mbele ni rahisi kuishi na kocha huyo huku pia akiwataka kujaribu kila wanapokaribia katika uso wa goli.

“Unaona kila wakati tunaangalia mbele anataka kuona tunapiga pasi zinazofika ukiweza kupiga ndefu zaidi ni hatua nzuri lakini iwe na uhakika,”alisema Tonombe.

“Anataka pia tupige mashuti pale tunapopata nafasi ya kupiga nafikiri ni kocha mzuri anayelenga kutaka matokeo nafurahi kufanya naye kazi.”

Kocha wa Mbeya City Amri Said ‘Stam’ amesema Yanga ya msimu uliopita na hii ya sasa ina tofauti kubwa.

Stam ambaye alikuwa beki wa mafanikio wa Simba miaka ya nyuma alisema Yanga sasa ina kikosi imara ambapo wachezaji wengi wana ubora wa kujua kutengeneza nafasi.

Bosi mkuu wa Yanga Dk Mshindo Msolla ameliambia Mwanaspoti kwamba usajili wao wa msimu huu ni wa mafanikio makubwa.

Msola ambaye kitaaluma ni kocha alisema katika wachezaji wao watano wa kigeni hakuna mtu mwenye mashaka na vifaa hivyo kwani pesa zilizotumiwa na wadhamini wao GSM zimetumika kihalali.

“Usajili huu ni mkubwa na kiukweli tangu niingie ndani ya uongozi safari hii naweza kusema tuna kikosi ambacho kitarudisha heshima yetu,”alisema Msola.

Akiwageukiwa wachezaji wazawa waliosajiliwa Msolla alisema nao wamethibitisha ubora wao ambapo kwa ambao hawakupata nafasi ya kuanza wanatakiwa kutambua hiyo ni hatua ya upana wa kikosi na kwamba wana nafasi ya kuzidisha mapambano ya kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Unajua hiyo ndio faida ya kuwa na upana wa kikosi yoyote ana nafasi ya kucheza muhimu ni juhudi zako kwenye mazoezi mpaka kwenye mechi siku ukipata nafasi.

“Ukiwachukua hawa wapya sasa ukawaunganisha na hawa waliowakuta utakuja kugundua kwamba msimu huu tuna timu bora sana,”aliongeza Msolla.

MSIKIE KASHASHA

Mchambuzi mkongwe wa soka, Alex Kashasha alisema; “Hataki mpira wa kutupa mbele anataka wacheze pamoja ukiwa na viungo kama Mauya (Zawadi) au mtu bora kama Tonombe au uwe na beki wa pembeni mwenye ubora kama ule wa Yassin au uwe na Shomari maana yake unazungumza una watu wanaojua kuusafirisha mpira kutoka nyuma kuja katika sehemu ya kiungo na kuupeleka mbele kwa utaratibu bora.”

“Ndio, kuna wakati kama timu mnaweza kutumia mpira wa kutupa mbele kulingana na mazingira ya mchezo au labda watu wawahi mbele huu ni mpira wa Kiingereza lakini huyu Krmpotic anatoka Serbia sasa hawa kwa kawaida wanapenda kucheza huru lakini wakiwa na nidhamu ya kutumia nafasi zaidi.

“Ukiangalia amewabadilisha haraka sana wachezaji ukimuangalia Mustapha huyu sio yule wa Polisi Tanzania angalia anavyocheza kwa maelewano bora na yule Kisinda kule pembeni. kuhusu ubora anasema.