Usiyoyajua kuhusu hawa makocha wa England

Muktasari:

  • Hata hivyo, kuna mambo ambayo huyafahamu kuhusu makocha wa EPL na hapa Mwanaspoti linakuchambulia kukuweka tayari na msimu ujao.

MSIMU wa Ligi Kuu England wa 2018/19 umeshakwisha ukiishuhudia Manchester City ikiweka rekodi ya kuwa, timu ya kwanza kutetea ubingwa wake, baada ya kipindi cha miaka 10. Mengi yametokea kwenye msimu huu yakiwemo ushindani na burudani.

Achana na ubabe wa Liverpool kwa Man City katika mbio za kuwania ubingwa. Achana na vita ya Top Four ambayo imeshuhudia panda shuka ya timu zilizokuwa zikichuana.

Achana na ubabe wa timu za England kwenye michuano ya Ulaya msimu huu. Hayo yalishapita na sasa watu wanajiandaa na msimu ujao, lakini wakati tukijiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu England. Ligi pendwa zaidi duniani na yenye kila aina ya mbwembwe kuanzia usajili, soka lake na upande wa makocha.

Hata hivyo, kuna mambo ambayo huyafahamu kuhusu makocha wa EPL na hapa Mwanaspoti linakuchambulia kukuweka tayari na msimu ujao.

UNAI EMERY

Safari yake ya ukocha Arsenal, ilianza kwa mafanikio. Amemaliza msimu na pointi nyingi kwenye EPL kuliko msimu uliopita. Kikubwa kwake ni ndoto ya kufuzu Ligi ya Mabingwa na kwa sasa iko hai kutokana na kufuzu fainali ya Europa League dhidi ya Chelsea.

Mafanikio ya Mhispania huyu katika michuano hii ya Europa, ni moja ya sababu za kupewa kazi pale Emirates. Hata hivyo, kiwango cha Washindi Bunduki hao kilikuwa cha mashaka sana katika mechi za ugenini, kwani wamepoteza mechi nyingi sana ugenini.

Hata hivyo, hili lilitarajiwa. Licha ya kuwa na mafanikio makubwa katika michuano hii, hasa akiwa na Sevilla, msimu wa mwisho wa Emery, kwenye ligi pale Ramon Sanchez Pizjuan, kabla ya kuhamia Emirates, haukuwa mzuri. Msimu wa 2015/16, Sevilla chini ya Unai Emery, ilimaliza kampeni yao kwenye La Liga, bila ya kupata ushindi hata mmoja katika mechi za ugenini. Walimaliza msimu katika nafasi ya saba, baada ya kupata sare tisa na kufungwa mara 10.

JURGEN KLOPP

Juni Mosi, mwaka huu kwenye dimba la Wanda Metropolitano, jijini

Madrid, Mjerumani Jurgen Klopp, ataingoza Liverpool kusaka taji lao la sita la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa mara ya pili mfululizo ikiwa ni fainali yake ya tatu kama kocha.

Mara yake ya kwanza kufanya hivyo, ilikuwa ni akiwa na kikosi cha Borussia Dortmund. Hata hivyo, mashabiki wengi wanafahamu msimu wa mwisho wa Klopp, pale Signal Iduna Park, ulivyomalizika.

Dortmund ilianza kwa kasi ya ajabu, kabla ya kuanza kuboronga na kumaliza katika nafasi ya saba, huku wakichapwa kwenye fainali ya German Cup. Katika mchezo wao wa mwisho walilimwa 2-1 na Werder Bremen. Historia itajirudia? Uswahiba wa Sean Dyche na Ian Woan. Hakuna asiyejua urafiki wa karibu ulioko kati ya Jurgen Klopp na kocha wa zamani wa Huddersfield, David Wagner. Lakini urafiki huu, haufikii uswahiba ulioko kati ya Kocha wa Burnley Sean Dyche na msaidizi wake Ian Woan.

Uswahiba wa wawili hawa ulianza tangu wakiwa wadogo, wakati huo wakichezea akademi ya klabu ya Nottingham Forest. Dyche alipokuwa kocha wa Watford, msaidizi wake alikuwa huyu huyu Woan. Walikuwa pamoja huko Watford pia.

Katika muda wote wanaokuwa kwenye majukumu yao pale Tur Moor, sio tu wanafanya kazi pamoja, bali pia wanaishi pamoja watu hawa, kwani kila mmoja ana familia yake nje ya Uingereza. Woan alikuwa mpambe ‘Bestman’ wa Dyche katika harusi yake.

Kitu kingine usichokijua, Dyche ambaye ndiye mdogo kati ya wawili hawa, alikuwa mpangaji kwenye nyumba anayomiliki Woan, wakati huo alikuwa ndio kaanza kazi.

Safari ya ukocha ya Pochettino

Ni nadra sana kusikia kocha fulani ana uzoefu kwa kucheza mechi kubwa. Mara nyingi wengi hujikuta wakiwa hawana uzoefu wowotewanapokabiliana na mechi yao ya kwanza, baada ya kukabidhiwa mikoba ya ukocha.

Hata hivyo, ni kawaida sana, kwa makocha kuwa na muda mwingi wa kufanya mazoezi na vikosi vyao, kabla ya kucheza mechi yao ya kwanza. Kwa Pochettino, mambo yalikuwa tofauti. Alikutana na Barcelona ndani ya saa 24 tu, ya kukabidhiwa kikosi cha Espanyol.

Muda mfupi baada ya kupata leseni yake ya UEFA ya kuwa kocha msaidizi wa timu ya wanawake, Murgentina huyo, aliteuliwa kukinoa kikosi cha wanaume, akiwa amefanya mazoezi mara mbili na timu yake, akakutana na Pep Guardiola.

Ilikuwa ni ngumu kuamini, lakini Pochettino aliamini na imani yake ikamwongoza kupata pointi moja mbele Barca ile ya kina Xavi na Iniesta. Mechi ikamalizika kwa sare ya 0-0. Huo ukawa mwanzo wa mzuri wa safari ya Poch anayesubiri fainali ya mabingwa.

Hakuna kama Nuno Espirito Santo

Nani ana swali kuhusu Nuno Spirito Santos? Ni kipi wanachokifanya makipa baada ya kustaafu? Makocha wa makipa au pia kurudi nyumbani.

Lakini ni wachache tu, kama Nuno Espirito Santo, ndio wanaofanikiwa kuwa makocha, kwenye ligi yenye ushindani kama EPL.

Bosi huyu wa Wolverhampton Wanderers, alisimama langoni katika vilabu vya ligi za Ureno na Hispania, kwa zaidi ya miaka 20. Alikuwa kipa msaidizi wa kikosi cha Porto cha Jose Mourinho, kilichotwaa ubingwa wa Ligi ya mabingwa mwaka 2004.

Baada ya kustaafu (2010), alihamia kwenye ukocha wa makipa, kabla ya kuwa kocha. Aliipandisha Wolves daraja na alichokifanya msimu huu, ni zaidi ya kilichofanywa na Nigel Adkins (2014), kabla ya kutimuliwa na Reading. Amewaacha wengi midomo wazi.

Sarri, Conte wapishana kiti

Maurizio Sarri alitua Darajani, msimu uliopita baada ya kufanya kazi adhimu akiwa na Napoli. Hii ilikuwa ni kazi yake ya kwanza nje ya

Italia akirithi mikoba ya mwenzake, Antonio Conte aliyetimuliwa. Hakuna jipya katika hilo. Makocha huajiriwa na kufutwa kazi. Lakini kwa Sarri na Conte sio mara ya kwanza. Mara ya kwanza, ilikuwa ni katika klabu ya Arrezo, mwaka 2006. Alianza kama kocha msaidizi, kabla ya kupewa majukumu kamili. Miezi mitatu baadaye, akapigwa chini na nafasi yake ikarithiwa na Sarri.