Usiwapimie stejini noma, uwanjani wanaupiga mwingi mno

NI kweli mshika mawili moja humponyoka, lakini asikuambie mtu kuna watu wenye bahati zao buana. Watu wa aina hiyo ni wale ambao wanaweza kuyafanya mambo mawili kwa wakati mmoja na kila kitu kikawa sawa.

Utabisha nini wakati Memphis Depay, licha ya kukinukisha uwanjani lakini pia anadili pia na muziki akiimba nyimbo zake katika miondoko ya hip hop.

Mholanzi huyu aliyewahi kukipiga klabu za PSV Eindhoven na Manchester United kabla ya kutimkia Olympique Lyon anayoichezea mpaka sasa, sio pekee kati ya watu waliojaliwa vipaji viwili na kuvitumia kwa wakati mmoja.

Miaka ya 1970 kwa mashabiki wa soka wanaukumbuka mziki wa Mayaula Mayoni, Mkongo aliyetikisa nchini akikipiga Yanga. Simba wanamkumbuka huyu jamaa ambaye pia alikuwa mahiri kwenye muziki wa Bolingo hasa ngoma yake matata ya ‘Mbongou’.

Mayaula ambaye sasa ni marehemu, kwa mashabiki wa Simba hawawezi kumsahau baada ya kuwalaza njaa kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe Karume baada ya kuwapiga mbili swaafi!

Mechi hiyo buana ilipigwa Juni 30, 1970 na Mayaula akatupia kambani katika dakika ya 32 na 36 kabla ya Omar Gumbo kuifungia Simba enzi hizo ikifahamika kama Sunderland bao la kufutia machozi dakika moja kabla ya pambano kumalizika.

Mwanaspoti linakuorodheshea baadhi ya wasanii ambao pia wanalikanyaga gozi la ng’ombe kama kawaida, kuonyesha kuwa kuna watu waliobarikiwa buana!

HUSSEIN MACHOZI

Achana na sauti yake ya mvuto katika maisha yake ya muziki, unaambiwa jamaa huyu ambaye majina yake kamili ni Hussein Rajab, alikuwa ni moja ya viungo mahiri, aliyewahi kukinukisha akiwa Kagera Sugar iliyomsajili kabisa baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari.

Machozi alisajiliwa na Kagera, lakini kutokana na kuvutiwa na kazi za kina Marlaw, Mr Blue, MB Dogg na wakali wengine akaanza kutunga nyimbo kabla ya kuchomoka jumla kwenye muziki.

Mwenyewe aliwahi kukaririwa akisema kilichomfanya atimke kwenye soka ni kwa vile kipindi anajiunga nayo, hakuona muelekeo wowote wa kumuinua kimaisha kulinganisha na muziki ambako alitamba na ngoma kadhaa za kusisimua ikiwamo ‘Kafia Ghetto’ aliyotoa mwaka 2007.

Hata hivyo, hivi karibuni, akiwa Kenya alikaririwa anawaonea wivu nyota wa sasa wa soka kutokana na ukweli wamekuwa wakitengeneza fedha za maana, japo alisisitiza hana mpango wa kulicheza soka kwa kuhofia kupigwa miba.

Kwa sasa Machozi, bado yupo nje ya nchi akiendelea na maisha yake huku akiwa hajaacha kabisa kufanya muziki.

TUNDA MAN

Mkali kutoka Tip Top Connection ambaye anakimbiza na ngoma zake kadhaa ikiwamo ‘Demu Sio’ na ‘Msambinungwa’ mbali na kazi zake za nyuma kama ‘Naila’, ‘Nipe Ripoti’ na nyinginezo, ni kati ya wasanii wenye sauti flani matata ambaye naye amevitumikia vipaji vyake viwili kwa wakati mmoja kabla ya kuamua kuchagua njia moja.

Ndio, kwa mashabiki wa Yanga, Tundaman kipindi hicho akiyatumia majina yake halisi ya Khaleed Ramadhan Tunda, jamaa alishakinukisha sana pale Kaunda kama kipa wa Yanga.

Unaambiwa jamaa katika harakati za kutafuta ugali alianza kucheza soka mara alipomaliza masomo yake ya sekondari pale Shule ya Forodhani, kisha kutua Yanga, mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini baada ya kuona mambo sio mambo aliamua kujikita zaidi katika muziki na kuachia ngoma yake ya kwanza ‘Neila’, aliyoshirikiana na Chid Benz na kumtambulisha rasmi kwa mashabiki.

Licha ya kubobea kwenye soka, lakini Tundaman bado amekuwa akionyesha kipaji chake kwa kusimama langoni tena akiwa nahodha wa timu ya Bongofleba kwenye matamasha mbalimbali na umahiri wake unaonyesha kama angekomaa, huenda angekula sahani moja na Juma Kaseja.

H-BABA

Kama unaikumbuka ile ngoma ya ‘Mpenzi Bubu’ na ‘Kuoga Lazima’, utajua ukali wa Hamis Ramadhani anayefahamika zaidi kama H Baba, mtoto kutoka jijini Mwanza.

Kama hujui, jamaa kabla ya kutumbukia kwenye muziki, kwanza alianza kama dansa akinengua sana tu kama Super Nyamwela, kiasi cha kuchukua ubingwa wa jijini Mwanza na kushiriki shindano la Disko Tanzania.

Achana na fani hiyo, mwimbaji huyu mwenye mwili jumba pia ni mmoja ya wasanii wanalijua soka kwa kulicheza akiwahi kusajiliwa Toto Africans na kuikosa kidogo kuwa miongoni mwa nyota wa Azam iliyotaka kumsajili 2011.

Mbali na kuimba na kucheza soka, H-Baba pia anaigiza filamu kuonyesha kuwa yeye ni zaidi ya wenzake kwani kokote anakinukisha kama kawaida.

Nafasi aliyokuwa akiicheza ni ushambuliaji na alikuwa akifunga sana tu kuanzia akiwa shuleni na ndio maana Kocha John Tegete mwaka 2012 aliamua kumsajili Toto, japo jamaa aliamua kutimkia kwenye muziki baada ya kuona fani hiyo inalipa zaidi kuliko kukinukisha uwanjani.

KR MULLAH

Nani hajui kazi ya KR Mullah a.k.a CD 700 aliyetamba na makundi mbalimbali ya muziki wa kizazi kipya likiwamo TMK Wanaume Family na baadaye Wanaume Halisi.

Majina yake kamili ni Rashid Ziada ‘Jibaba’, amekuwa akifananisha na nyota wa zamani wa Arsenal, ‘Gervinho’.

Amezichezea timu kadhaa wilayani Temeke ikiwamo Sumu ya Mamba na Inter Milan, Gaza FC zilizokuwa zikishiriki Ligi Daraja la Tatu na Nne sambamba na michuano ya Ndondo kabla ya kubadili upepo na kutumbukia kwenye muziki akianzia na GWM Mazimwi.

Alikuwa mchezaji kiraka mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kuanzia kiungo, winga na mshambuliaji na aliitwa Zico kutokana na uwezo wake.

ALIKIBA

Wengi wamekuja kushtuka wakimuona anacheza soka katika klabu ya Coastal Union iliyopo Ligi Kuu Bara katika msimu uliopita.

Lakini ukweli jamaa ni mchezaji wa muda mrefu na amekuwa akishiriki mechi mbalimbali za Ligi Daraja la Tatu wilayani Ilala na kuna kipindi alitakiwa kusajiliwa na African Lyon lakini alipotezea ofa hiyo na kuendelea na maisha ya muziki.

Kiba ambaye majina yake kamili ni Ali Saleh Kiba, hakupata muda mwingi wa kucheza Ligi Kuu sababu ya ubize wa muziki, ila alionyesha anaujua kwenye zile mechi za hisani za taasisi yake na Mbwana Samatta.