Ushindi wa Sudan waipandisha Tanzania viwango Fifa

Muktasari:

Viwango vya ubora wa Fifa hutolewa kila mwezi kulingana na mafanikio ya nchi kwenye soka katika mwezi husika

Dar es Salaam. Tanzania imepanda kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa mwezi Oktoba vilivyotolewa leo.

Awali Tanzania ilikuwa nafasi ya 135 na sasa imepanda hadi nafasi ya 133 baada ya kukusanya pointi 1084 ndani ya Oktoba.

Sare ya bila kufungana na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Sudan kwenye mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) yameonekana ni matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kupanda kwa Tanzania kwenye viwango hivyo vya ubora vya FIFA kwa mwezi huu.

Wakati Tanzania ikipanda kwa nafasi mbili, Uganda wameendelea kuwa wababe wa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kwa sasa wapo nafasi ya 79 ikimaanisha wamesogea juu kwa nafasi moja kutoka ile ya 80 waliyokuwepo awali huku Kenya ikiwa ya pili kwa ukanda huu kwani ipo nafasi ya 108 ikiwa ni anguko la nafasi moja.

Rwanda imepaa kwa nafasi moja kutoka ile ya 130 hadi ya 129 wakati Burundi yenyewe imepanda kutoka nafasi ya 144 hadi ile ya 143.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa ukanda wa Afrika Mashariki, nchi tatu ambazo zimepangwa kundi moja na Tanzania kwenye mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 ambazo ni Tunisia, Guinea ya Ikweta na Libya zenyewe zimeshindwa kusogea juu kutoka kwenye nafasi zilizokuwepo mwezi uliopita.

Tunisia imebakia kwenye nafasi yake ileile ya 29 ambayo ilikuwepo awali wakati Libya imeporomoka kwa nafasi moja kutoka ile ya 102 hadi ya 103 wakati Guinea ya Ikweta nayo imeanguka kutoka nafasi ya 134 hadi ile ya 135.

Nafasi nne za juu kwenye viwango hivyo hazijabadilika ambapo, Ubelgiji inaongoza, ikifuatiwa na Ufaransa, Brazil na England na Ureno iliyokuwa nafasi ya tano, imeporomoka hadi nafasi ya sita, ikipishana na Uruguay ambayo imepanda kwa nafasi moja.

Nicaragua na Sudan Kusini zenyewe ndio timu ambazo zimepanda kwa nafasi nyingi zaidi juu wakiwa wamefanya hivyo kwa nafasi 11 kila moja.

Nicaragua wamepanda kutoka nafasi ya 148 hadi ya 137 wakati Sudan Kusini wamepnda kutoka nafasi ya 173 hadi ya 162.

Mauritius ndio timu iliyoanguka kwa nafasi nyingi zaidi ambapo imedondoka kwa nafasi 12 kutoka ile ya 161 hadi nafasi ya 173.