Ushindi kidogo Mawenzi yaanza kuchonga

Muktasari:

Ligi Daraja la Kwanza ndiyo imeanza huku Mawenzi ikiwa imecheza mechi mbili hadi sasa wakifungwa moja na kushinda moja

Morogoro. Mawenzi Market FC imewasha mitambo baada ya kuichapa Kiluvya United kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Ushindi huo unaifanya Mawenzi Market FC kupata pointi tatu baada ya mchezo wa kwanza kuambulia kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa Mufindi United ya Iringa.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Mawenzi Market FC, Hassan Mbande alifunga mabao yote mawili na kuamsha shangwe kwa mashabiki wao.

Safu ya ulinzi ya Kiluvya United FC ilishindwa kumdhibiti kiungo mshambuliaji, Seleman Kibadeni aliyekuwa nyota kwa kutawala eneo la kiungo na kutoa pasi za mwisho kwa mfungaji.

Mbande alifunga bao la kwanza katika dakika kwanza akiwazidi maarifa walinzi wa Kiluvya United huku bao la pili akifunga katika dakika ya 66.

Kocha Mkuu wa Mawenzi Market FC, Mussa Rashid alisema ushindi huo umeamsha ari baada ya mchezo wa kwanza kupoteza dhidi ya Mufundi United.

Rashid alisema wachezaji na benchi la ufundi wanaelekeza akili katika mchezo ujao dhidi ya Majimaji FC mjini Songea ili kwa lengo la kupata ushindi utakao waweka kileleni mwa msimamo wa kundi lao.

“Tumewasha mitambo yetu rasmi mbele ya Kiluvya United kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 na sasa tunaelekeza nguvu, akili na mbinu kwenye mchezo wa tatu ugenini dhidi ya MajiMaji FC,”alisema Rashid.

 

Kocha Mkuu wa Kiluvya United, Bakari Besti alisema wamepoteza mchezo huo kutokana na wachezaji wengi kukosa uzoefu.

Besti alisema mchezo wa mpira ni mchezo wa kigeugeu kwani katika mchezo na Ashanti United wachezaji wake walicheza vizuri na kutoa sare, lakini ameshangazwa kuona kiwango dhidi ya Mawenzi Market kwa kucheza chini ya kiwango.