Usajili Simba, Yanga umenoga

Muktasari:

Awali Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans Pluijm alizifundisha klabu za Yanga, Singida United na sasa Azam FC kwa Tanzania lakini ana uzoefu na soka la Afrika baada ya kukaa kwa kipindi kirefu nchini Ghana.

Dar es Salaam.  Dirisha la usajili linafunguliwa rasmi kesho Alhamisi Novemba 15, na wakati muda huo ukikaribia vurugu za kugombea wachezaji zimeshaanza mapema tu.

Kama ilivyo kawaida kwa timu za Simba, Yanga na Azam FC mdogo mdogo wanafanya yao wakisaka wanaoweza kuwafanyia mambo.

Azam imekuwa ya kwanza kumdaka mshambuliaji Mzambia Obrey Chirwa waliyemsajili akitokea Klabu ya Nogotoom ya nchini Misri.

Aliyekamilisha usajili huo ni kocha mkuu wa kikosi hicho, Mholanzi Hans Pluijm ambaye alimfundisha wakati anaichezea Yanga.

 

WAWILI WANATINGISHA

Mshambuliaji wa Ndanda FC, Vitalis Mayanga anadaiwa kuwa muda wowote atasajiliwa na Yanga, lakini kutokana na kubanwa na majukumu ya mkataba na timu yake hiyo ya Mtwara, kumbana vijana wa Jangwani wanatakiwa kufanya kazi ya ziada katika kuvunja mkataba wake.

Mchezaji mwingine ni Eliud Ambokile wa Mbeya City anayetakiwa na klabu za Simba na Yanga.