Usajili wa Morrison ... Eymael amaliza ubishi

Muktasari:

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti limezipata ni kwamba mmoja wa vigogo wazito wa Simba alishamshikisha Morrison Dola 10,000 (Sh23 milioni) kwa makubaliano kwamba watampa Dola 40,000 (zaidi ya Sh90 milioni) wakati ukifika ili wamalize dili.

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael ameivutia waya Mwanaspoti kutoka Ubelgiji na kuwasisitizia mashabiki wa klabu hiyo kwamba waachane na uzushi wa Benard Morrison kusaini Simba.

Eymael ameweka wazi kwamba katika vitu ambavyo amepambana kuhakikisha GSM wanaviweka sawa mapema ni usajili wa mchezaji huyo aliyefunga bao pekee kwenye mechi ya watani hivi karibuni na kuwapa Yanga cha kuongea mitaani.

Amesema akiwa katika majukumu yake mengine nyumbani kwake Ubelgiji, aliwasiliana na mmoja wa wakurugenzi wa GSM, Hersi Said na kumhakikishia kwamba wamemsainisha mkataba wa miaka miwili na ataendelea kuwa naye kwa misimu miwili ijayo.

“Baada ya kupewa taarifa hizo nilimtafuta na mchezaji mwenyewe Morrison ambaye naye yupo mapumziko, na alikubali kwa kuniambia amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga baada ya kufikia makubaliano na GSM ambayo yalianza siku nyingi nyuma hata kabla ya ligi kusimama.

“Kama kuna habari au taarifa nyingine tofauti na hiyo sidhani kama inaweza kuwa na ukweli wowote kutokana Hersi Said, kunitumia picha za mkataba wa Morrison na hata zile akiwa anasaini, kwa maana hiyo tutaendelea kuwa naye msimu miwili mbele.

“Unajua wachezaji kama Morrison ambao wanaonyesha uwezo wa hali ya juu huku mkataba wake ukiwa umemalizika lazima atanyemelewa na timu nyingine, kwa maana hiyo hilo suala la Simba au timu nyingine kumtaka hauwezi kulizuia, lakini jambo sahihi ambalo wapenzi wa Yanga wanatakiwa kulifahamu Morrison amesaini miaka miwili katika timu yao,” alisema Eymael.

“Unajua ili Yanga waweze kufanya vizuri kama ambavyo wanahitaji lazima kikosi kiwe na wachezaji aina ya Morrison wengi, kwa maana hiyo unamuacha vipi mchezaji kama huyu anakwenda katika timu nyingine ingekuwa ngumu.”

“Niwapongeze viongozi kwa kuanza kuifanyia kazi ipasavyo ripoti yangu kwa kufanikisha zoezi la kumbakisha Morrison ambaye nina imani kama tukipata wachezaji wengine wa aina yake katika usajili wa dirisha kubwa tutapiga hatua zaidi,” aliongeza Eymael ambaye tangu atue Yanga usajili wa mkono wake ni Morrison pekee kwenye dirisha dogo.

MILIONI  23 ZATAJWA

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti limezipata ni kwamba mmoja wa vigogo wazito wa Simba alishamshikisha Morrison Dola 10,000 (Sh23 milioni) kwa makubaliano kwamba watampa Dola 40,000 (zaidi ya Sh90 milioni) wakati ukifika ili wamalize dili.

Ingawa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ameiruka kabisa ishu ya Morrison kwa madai kwamba haijui, lakini Mwanaspoti linajua kuwa ni ishu iliyokuwa inafanywa kimyakimya sana ili iwe sapraizi kwa mashabiki, lakini ikabuma na mchezaji husika amewaambia viongozi wa Yanga kwamba kuna mkwanja kavuta sehemu ila ataurudisha.