Usajili wa Man United ni tishio

Muktasari:

  • Ripoti za kutoka Nou Camp zinadai Barca inaweza kukubali kumpiga bei staa huyo aliyemnasa kwa Pauni 142 milioni Januari mwaka jana tu hapo, ili wachangishe pesa ambazo zitatosha kufanya usajili mwingine wa maana, ikiwamo wa kumrudisha Neymar kwenye chama lao.

MANCHESTER, ENGLAND.ANAKUJA au haji? Hayo ni maswali yanayowatawala mashabiki wa Manchester United kwa sasa juu ya supastaa wa Barcelona, Philippe Coutinho.

Unaambiwa hivi, kwenye soka lenye kutumia pesa, chochote kinaweza kutokea hasa kama Barcelona wenyewe wakiwa tayari kufanya biashara.

Ripoti za kutoka Nou Camp zinadai Barca inaweza kukubali kumpiga bei staa huyo aliyemnasa kwa Pauni 142 milioni Januari mwaka jana tu hapo, ili wachangishe pesa ambazo zitatosha kufanya usajili mwingine wa maana, ikiwamo wa kumrudisha Neymar kwenye chama lao.

Ugumu uliopo Coutinho ambaye amekuwa akiwekwa benchi na Kocha Ernesto Valverde anataka kupambana na kupata namba kwenye kikosi hicho baada ya kuona Ousmane Dembele akipewa nafasi zaidi. Wakati anatua Nou Camp, Coutinho alisema amejiunga kwenye timu ya ndoto zake, hivyo suala la kukubali kuondoka kwenye timu hiyo kirahisi litakuwa gumu. Lakini kuna kitu kinaitwa pesa, ambacho kinaweza kubadili sura ya mchezo muda wowote ule.

Kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, chochote kinaweza kutokea na kama Barcelona itafungua milango, basi Man United inaweza kufanya mchakato wa kumbeba Mbrazili huyo, aliyewahi kuwatumikia mahasimu wao wa Ligi Kuu England, Liverpool. Kwenye dirisha lijalo la usajili huko Ulaya, Man United ina sura za mastaa wengi inaohitaji kuwaingiza kwenye kikosi chake licha ya kwamba jambo hilo linaweza kuwasababisha pia kupoteza baadhi ya wakali wake akiwamo Alexis Sanchez na Paul Pogba. Ripoti zinadai Man United inataka kupunguza bili ya mishahara kwenye kikosi chake na hilo linaweza kuifanya ikubali kirahisi kuwafungulia mlango wa kutokea Sanchez na Pogba, huku ikilenga kwenye kuwakamata mastaa kama Douglas Costa na Coutinho. Wachezaji wengine inayowataka Man United, ambao haitavunja benki yake kwenye kuwalipa mishahara kila wiki ni mabeki Eder Militao, Kalidou Koulibaly na Toby Alderweireld, huku kwenye kiungo ni Douglas Costa, James Rodriguez, Adrien Rabiot, Coutinho na Axel Witsel. Kuhusu Douglas Costa ni kwamba Juventus imewaambia wazi Man United kama inamtaka mchezaji huyo, basi iwape Pogba, dili ambalo linadaiwa linaweza kutokea mwishoni mwa msimu. Lakini kila kitu kinaelezwa kitafanyika kama tu Man United itaachana na Kocha Ole Gunnar Solskjaer mwishoni mwa msimu na kumleta kocha mwingine kwa sabababu kama Ole akibaki, basi Pogba haonekani kama atahama Old Trafford.

Wengine kwenye rada ya United ambao haitashangaza wakionekana kwenye kikosi hicho msimu ujao ni winga Ivan Perisic na Gareth Bale, huku kasi ya timu hiyo kwenye kushinda mechi zake ikipewa nguvu kubwa ya kubeba mastaa wa maana mwishoni mwa msimu.