Usajili wa JKT Tanzania kwa raha zao

Muktasari:

  • Kikosi cha JKT Tanzania kimekamilisha usajili wa wachezaji sita na sasa kinasumbua kichwa kumpata beki wa kati ambaye wanamuwinda kila kona.

Dar es Salaam. Maafande wa JKT Tanzania wamenasa saini za wachezaji sita kati ya saba wanaowahitaji ndani ya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Abdallah Mohammed 'Bares' tayari kimewasajili, Danny Lyanga, Hafidh Mussa, Adam Adam, Khomeny Khaluphan, Jabir Aziz na Adeyum Saleh.
Kwa sasa imebakisha nafasi ya mchezaji mmoja ambaye ni beki wa kati, ili kukamilisha idadi hiyo.
Bares amesema, mipango yao ya usajili imekwenda vizuri na watakapokamilisha usajili wa nafasi hiyo  kila kitu kitakwenda sawa.
"Sehemu kubwa ya usajili wetu ni kama tumeukamilisha baada ya kuwapata wachezaji tunaowahitaji. Tumefanikiwa kuwapata sita na sasa imebaki nafasi moja kulingana na mipango yetu,"alisema Bares.
Bares alimaliza msimu na JKT Tanzania ambayo baadaye ilimwongezea mkataba mpya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.