Usajili haukumuacha salama beki Mwadui

Muktasari:

  • Mgunga alisema kazi yake ni mpira na hachagui timu isipokuwa anachohitaji ni mazingira mazuri ili kutimiza majukumu yake.

Mwanza. Beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga amejiunga na klabu ya Gwambina FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Mchezaji huyo aliyeisaidia Mwadui kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara, anakwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Katibu Mkuu wa Gwambina, Daniel Kirahi alithibitisha kumnasa beki huyo wa kati na kueleza kuwa msimu ujao nyota huyo atakuwa katika uzi wao.

Alisema wamenasa nyota wengine Yusuph Kagoma wa Singida United na kipa Ibrahim Isihaka kutoka Alliance FC.

“Tumedhamiria kufanya usajili wa maana tukilenga kupanda Ligi Kuu, usajili hauishii hapo kuna vifaa vingine tunasubiri taratibu zikamilike wavae uzi mpya,”alitamba Kirahi.

Mgunga alisema kazi yake ni mpira na hachagui timu isipokuwa anachohitaji ni mazingira mazuri ili kutimiza majukumu yake.

“Ninahitaji kucheza mpira kwa sababu hata Gwambina FC tutaipandisha kwahiyo naenda kupambana,”alisema beki huyo.