Usajili CAF pasua kichwa Msimbazi

Muktasari:

  • Ugumu wa kwanza ni kwamba Simba ina wachezaji 10 wa kigeni ambapo wamedai ili kikosi kiwe bora na kutimiza malengo usajili wao wanatakiwa kusajili mchezaji wa kigeni kwa mujibu wa viongozi.

KASI ya wapinzani wao wa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kusajili majembe ya maana kuelekea mechi za kundi hilo, imewapa presha mabosi wa Msimbazi, wakikiri usajili huo wa CAF kwao ni pasua kichwa wakikwazwa sehemu mbili tu.

Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DR Congo zilizopangwa kundi moja na Simba zimekuwa zikifanya usajili wa kutisha kuelekea mechi zao, jambo ambalo limezidi kuwapa presha viongozi wa Simba.

Mabosi wa Simba wamefichua, endapo kocha wao, Patrick Aussems anataka kusajili mchezaji kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wapo tayari lakini ugumu upo sehemu mbili.

Ugumu wa kwanza ni kwamba Simba ina wachezaji 10 wa kigeni ambapo wamedai ili kikosi kiwe bora na kutimiza malengo usajili wao wanatakiwa kusajili mchezaji wa kigeni kwa mujibu wa viongozi.

Pili imeelezwa kupata mchezaji ambaye hajacheza mechi za michuano hyo ambaye ni bora zaidi napo ni kazi kubwa hata kama usajili ungekuwa unafanywa sasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentus Magori aliliambia Mwanaspoti kisiwani hapa, wanatamani kufanya hivyo ila wanakutana na vigingi hivyo wanamuachia kocha wao kama atakuwa na mapendekezo mengine.

“Kikao kilichopita tulijadili mambo mbalimbali, ila suala la usajili bado linatupa wakati mgumu kwani nafasi za wachezaji wa kigeni zimejaa na hatuwezi kupunguza mtu kwa sasa, pia kupata mchezaji mzuri ambaye hajacheza michuano hii nayo ni kazi nyingine.

Hivi karibuni, Simba ilikuwa ikimnyemelea straika wa Nkana, Walter Bwalya lakini kwa kanuni za CAF isingekuwa rahisi kumsajili kipindi hiki kwani asingekuwa na msaada kwao maana amecheza mechi za ligi hiyo ambayo ndiyo malengo yao makubwa.

Wakati mipango ya Simba ikionekana kuwa migumu kidogo, wapinzani wao wa Al Ahly ndani ya muda mchache wameshusha Hussei El Shahat kutoka nyota wawili kutoka klabu ya Al Ain ya Falme za Kiarabu, Ramadan Sobhi waliomrejesha kwa mkopo kutoka Huddersfield ya England.

Al Ahly pia imewasajili Mohammed Mahmoud aliyekuwa akiichezea klabu ya Wadi Degla ya Misri, Muangola mwenye uraia wa Brazili Geraldo kutoka 1st Do Agosto ya Angola na Mahmoud Wahid kutoka El Makasa ya Misri.

JS Saoura yenyewe imemnasa nyota wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu na straika Rafik Boukbouka kutoka US beni Douala ya Algeria na winga Ziri Hammar, huku AS Vita ikimsainisha beki matata raia wa Uganda, Savio Kabugo na wengine kama sehemu ya kuimarisha vikosi vyao kwaaji ya mapambano.