Upo hapo? Maguire uso kwa uso na Vardy, Arsenal zamu yao kesho

Muktasari:

Leicester haijapoteza mechi yoyote kati ya nne ilizocheza kwenye ligi msimu huu, huku Maguire na timu yake mpya, ameshachapwa mara moja, akitoka sare mbili na kushinda mara moja tu.

LONDON, ENGLAND.UTAAMBIA nini watu? Harry Maguire leo Jumamosi atakuwa na kibarua cha kuwakabili waajiri wake wa zamani huko uwanjani Old Trafford, huku akiambiwa tangu aondoke, hajawahi kuwa pengo.

Leichester City ilimpiga bei Maguire kwenda Manchester United kwa ada ya Pauni 80 milioni na timu hizo mbili zitakumbana leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaofanyika uwanjani Old Trafford.

Wakati Maguire anaondoka Leicester City, maswali yalikuwa mengi Brendan Rodgers atafanyaje, lakini jambo hilo halijawahi kuwa tatizo, kwani kocha huyo amekijenga kikosi chake na kukifanya kuwa bora zaidi.

Leicester haijapoteza mechi yoyote kati ya nne ilizocheza kwenye ligi msimu huu, huku Maguire na timu yake mpya, ameshachapwa mara moja, akitoka sare mbili na kushinda mara moja tu.

Maguire ana shughuli pevu leo ya kuwakabili Maddison, Youri Tielemans na Jamie Vardy, ili Man United isikumbane na aibu, wakisaka ushindi wa kwanza tangu mwanzo wa msimu, walipoichapa Chelsea Bao Nne. Hii inaitwa usiyempenda kaja!

Kipute hicho cha Old Trafford ndicho kinachosubiriwa kwa hamu wikiendi hii, ambapo Kocha Ole Gunnar Solskjaer ametangaza majeruhi kibao kwenye kikosi chake akiwamo Paul Pogba, Anthony Martial, Luke Shaw, Jesse Lingard, Eric Bailly, Diogo Dalot na Aaron Wan-Bissaka, ambao wote wapo kwenye hatihati kucheza mchezo huo.

Ligi hiyo inayorudi upya wikiendi hii baada ya mapumziko ya mechi za kirafiki, itaishuhudia Liverpool pia ikisaka rekodi yake tamu ya mwanzo wa msimu wakati itakaposhuka uwanjani Anfield kuikabili Newcastle United. Liverpool imeshinda mechi zake zote nne ilizocheza kwenye ligi hadi sasa, hivyo itasubiri kuona kama itaendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 itakapoikabili Newcastle huko Anfield.

Mabingwa watetezi, Manchester City watakuwa ugenini kwa Norwich City, kujaribu kufuta pengo la pointi lililopo baina yake na Liverpool.

Man City inashika nafasi ya pili kwenye msimamo, pointi mbili nyuma vinara Liverpool.

Katika mchezo huo, Kocha Pep Guardiola atakosa huduma ya beki wake wa kati, Aymeric Laporte akiamini John Stones atamaliza matatizo kwenye safu ya ulinzi ya wababe hao wa Etihad. Kwingineko, Brighton itakuwa na kibarua kigumu cha kuikabili Burnley.

Tottenham Hotspur, ambao kocha wake, Mauricio Pochettino amewakalisha kitako mastaa wake wanaotaka kuondoka, akiwamo kiungo Christian Eriksen, kutuliza akili yao na kuisaidia timu hasa katika mchezo wa leo kuikabili Crystal Palace ya supastaa, Wilfried Zaha.

Chelsea, ambayo inajaribu kujiweka sawa chini ya kocha wake, Frank Lampard itakuwa ugenini kwa Wolves, wakati Sheffield United itakuwa nyumbani kuikaribisha Southampton.

Lampard anajaribu kukifanya kikosi chake kusaka ushindi wa pili msimu huu baada ya kushinda mara moja tu, akitoka sare mbili na kuchapwa mara moja katika michezo minne iliyocheza, huku ikiwa imejikusanyia pointi tano na kushika nafasi ya 11 kwenye msimamo.

Pochettino anafahamu wazi Palace wamekuwa wagumu msimu huu, amkwa sasa wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kuvuna pointi saba katika mechi nne, huku Solskjaer na chama lake la Man United wakifahamu shida wanayokwenda kuikabili mbele ya Leicester City, inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa.