Upangaji matokeo ama rushwa FDL

Muktasari:

  • FDL ina matatizo mengi sana hususani haya ya rushwa....naomba nitoe ushuhuda mmoja labda nitatoa mwanga fulani.

USIKU wa Ijumaa ya Februari 8, zilisambaa picha zikimuonesha Katibu Mkuu wa Dodoma FC, Fortunatus Johnson, akifanya jaribio la kumhonga mchezaji wa Rhino Rangers ya Tabora. Februari 9, TFF ikatoa taarifa rasmi kwamba wamepata taarifa ya tukio hilo na wanalifanyia kazi.

Taarifa hii ikamuibua kipa wa zamani wa klabu moja maarufu ya mjini Morogoro, Abel Cosmas Ndongo maarufu kama Kaike na kutoa ushuhuda wake kwa aliyoyaona wakati akichezea timu hiyo.

SIMULIZI LENYEWE

FDL ina matatizo mengi sana hususani haya ya rushwa....naomba nitoe ushuhuda mmoja labda nitatoa mwanga fulani.

Nikiwa katika timu fulani ya Daraja Kwanza ya mkoani Morogoro katika msimu ambao alipanda Mwadui, tulikutana na mambo mengi sana ambayo kiukweli sio mazuri.

Nilisajiliwa ile timu nikiwa kipa peke yangu katika raundi ya pili kwa sababu timu ile ilikuwa mkiani na wachezaji wengi waliondoka kutokana na ukata, hivyo hadi nafika pale nikakuta timu ina wachezaji 14 tu.

Nashukuru Mungu tulipambana sana kwa mechi nne tulizocheza uwanja wa nyumbani (Jamhuri) tulishinda hivyo tukapanda nafasi mbili juu.

Kizaazaa kilianza mechi yetu dhidi ya (jina tunahifadhi) iliyokuwa mkiani, mechi ambayo ilipangwa kufanyika Uwanja wa Karume.

Uongozi (katibu) alitupa taarifa mechi ni Jumatano, nasi tukajiandaa kwa ajili ya mechi hiyo. Siku ya Jumanne majira ya saa nne asubuhi, mlezi wa timu yetu ambaye ni Diwani wa Kata ya Mji Mpya (Mr. Nyau) alipigiwa simu na watu wa TFF kuwa mbona viongozi wa timu yetu hawaonekani kwenye mkutano wa kabla ya mechi (PM).

Mheshimiwa Diwani alitaharuki kwa kuwa naye aliambiwa na katibu kuwa mechi ni Jumatano, kumbe si kweli.

Mhe. Diwani akafanya jitihada za kutafuta usafiri na wachezaji, saa sita tukaanza safari ya kwenda Dar es Salaam wakati mechi ni saa kumi.

Kwa kibali cha RTO (Mkuu wa Usalama Barabarani) tulisafiri kwa haraka sana ili tuwahi mechi, hadi kufikia saa kumi kasoro dakika 5 tupo Airport kwa kuwa tulipitia njia ya Mbezi - Kinyerezi.

Kutokana na foleni kubwa sana ya magari ikatulazimu tushuke na kukodi bodaboda moja watu wawili. Tulifika Karume saa kumi na robo tukakuta wapinzani wameshakaguliwa na kupasha misuli.

Kwa kuwa tulikuwa tumeshavaa tukiwa garini, ikabidi tuingie uwanjani, tena tukiwa na njaa kubwa. Hatimaye kipindi cha kwanza tukafungwa goli 3. Tukiwa mapumziko, akatokea mdau mmoja akatununulia yale matunda mchanganyiko ya elfu moja moja, tukala. Tulipokuja kuingia kipindi cha pili, tukajitahidi tukarudisha goli mbili lakini muda nao ukawa umeisha tukamaliza mechi tumefungwa 3-2. Baada ya mchezo huo tukagundua janja iliyofanyika, kumbe wapinzani wetu walimpa pesa katibu ili asilete timu uwanjani ili sisi tushushwe daraja na wao wasalimike kwa kuwa wao ndo walikuwa mkiani.

Ndani ya gari tukiwa njiani kurudi Morogoro ulitokea ugomvi mkubwa sana baina ya wachezaji na katibu, hali iliyopelekea sisi kama wachezaji kuamua kumshusha katibu njiani.Baada ya hapo tukasafiri kuelekea Tabora kucheza na (jina pia tumehifadhi) tukapoteza kwa goli 1 la penalti (mazingira yale yale ya kwanza, mlungula ulitumika), halafu tukaenda Arusha kucheza na klabu ya JKT Oljoro tukatoka 1-1. Baada ya hapo tukaenda Moshi kucheza na klabu ya (jina tulihifadhi)...hapo pia tukagundua mengine mazito. Baada ya mechi ile kuisha kwa 0-0, baadhi ya viongozi wa timu pinzani wakamzingira kocha wetu (jina kapuni) na kudai warudishiwe pesa zao. Tukaingilia kujua nini tatizo, tukagundua kuwa kumbe kocha alichukua pesa ya kwa wapinzani wetu ili tufungwe. Kutokana na tamaa yake, hakutaka kumshirikisha mtu yeyote katika hilo, akiamini kwamba tutapoteza na yeye ataweka mpunga mfukoni, kitu ambacho kikawa tofauti. Ulitokea ugomvi mkubwa baina yetu na watu wa timu pinzani, ikalazimu ile pesa (laki moja) tugawane halafu tusilale moshi kwa kuhofia usalama wetu. Tuliumia sana kuwa pamoja na kupambana kwetu tena hatuna mishahara wala posho zaidi ya kugawana mapato ya getini (gate collection), kumbe ndani ya timu kuna watu wanatuhujumu, tuliumia sana.

Baada ya hapo tukapata uhakika wa kubaki daraja la kwanza, huku tukiwa tumebakiza mechi moja na timu ya (jina nalo tumehifadhi) iliyokuwa ikifanyika Shinyanga. Hapo napo ilikuwa kivumbi kwa sababu ni wapinzani wetu na klabu ya (jina kapuni) ndio waliokuwa wakiwania kupanda Ligi Kuu. Ile timu nyingine walianza kuongea na sisi ili tuwakazie wapinzani tuliokuwa tunacheza nao kwao kwa ahadi ya milioni 3 ambazo watatupa baada ya mechi. Tukasafiri hadi Shinyanga, kumbe huku nyuma Kocha wa wapinzani wakati huo (jina kapuni) alituma Sh 3 milioni kwa kiongozi mwingine ambaye hakusafiri na timu, naye hakutuambia lolote akaziweka mfukoni kwake.

Tumefika Shinyanga tu asubuhi siku ya mechi, kutokana na hali ya uchumi ya timu yetu, tukachukua nyumba ya kulala wageni ya hali ya chini sana. Baada ya muda mfupi yule kocha akaja akiwa ameongozana na wachezaji wake wakubwa tu watatu (majina kapuni), kwa bashasha wakatutafutia lodge nzuri zaidi tukahama.

Baadaye kwenye mazungumzo tukagundua kuwa alituma milioni 3, lakini kwa kuwa sisi kama wachezaji hatukuzipata ikabidi tugome kuuza mechi kwa sababu kiongozi yule aliyetumiwa pesa zile alizima simu kabisa baada ya kupigiwa. Kocha yule na wale wachezaji wake wakatoka wakiahidi kwenda kutafutia pesa nyingine na kuahidi kurudi baada ya muda mfupi. Kweli baada ya saa moja kocha yule alirudi na milioni mbili akiahidi hiyo moja iliyobaki atatumalizia tukifika uwanjani. Muda wa mchezo ulipofika tukaanza mechi, hadi kipindi cha kwanza kinaisha tukawa tumefungwa 2-0 huku tukiwa tumepanga kikosi dhaifu.

Wakati wa mapumziko tukaenda kuulizia pesa yetu iliyobaki tukaanza kuzungushwa tu, ikabidi tuingie kipindi cha pili na tukafanya mabadiliko, wakaingia wachezaji muhimu na Mungu si Athumani hadi kufikia dakika ya 73 tukawa tumerudisha goli zote mbili. Taharuki kubwa ikatokea uwanjani kwa sababu kwanza wananchi wote waliingia bure ili kuisapoti timu yao na uongozi mzima wa Mkoa wa Shinyanga ulikuwepo pale. Kocha yule akatafuta milioni moja haraka sana akatukabidhi basi nasi tukakubaliana tuwaachie. Dakika ya 85 mchezaji wetu akaudaka mpira makusudi ndani ya eneo la 18 na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti, hivyo wapinzani wetu wakapata goli la 3 na mechi ile ikaishia hapo hapo kabla hata ya dakika 90 hazijakamilika, hivyo wenyeji wetu wakawa wamepanda rasmi daraja, huku sherehe kubwa ikifanyika uwanjani hapo na sisi tukijumuika nao. Wenzetu wakifurahia kupanda daraja na sisi tukifurahia milioni 3.

Jioni kwenye sherehe yao tukaalikwa, tukala na kusaza kabla ya kesho yake alfajiri kuanza safari ya kurudi Morogoro.

Baada ya hapo kila mchezaji aliondoka kwenye timu ile kwa sababu ilikuwa ikiendeshwa kihuni sana na sasa hivi kwa taarifa nilizonazo nasikia imeshuka hadi daraja la 3 na bado haifanyi vizuri. Hivyo niliyowapa ndio picha halisi ya FDL, kuna michezo mingi sana michafu katika ligi hiyo sema tu basi!