United mpo? Auba anakuja huyo

LONDON, ENGLAND. SUPASTAA wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amesema ana uhakika ataanza kufunga mabao kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United utakaopigwa Old Trafford leo Jumapili.

Vichapo vya bao 1-0 mfululizo kwenye ligi vimepoozesha mwanzo mzuri wa Arsenal wakati wakiwa na safari hiyo ya kwenye Old Trafford kwenye mchezo mgumu.

Lakini, kiwango cha nahodha huyo kwa mechi za karibuni tangu alipopewa mkataba mpya kimeanza kuwapa shaka mashabiki, akiwa amefunga bao moja tu kwenye ligi.

Hata hivyo, mwenyewe alisema hana muda mrefu ataanza kutikisa nyavu kama ilivyokuwa awali.

“Kwa sasa kufunga mabao kumekuwa kugumu sana. Hii inatokea kwenye timu — sijafunga bao katika mechi kadhaa za ligi,” alisema.

“Lakini, sisi timu yenye uzoefu, tuna washambuliaji wenye uzoefu, hivyo hili jambo la kufunga litakwisha tu. Mimi sina shaka kabisa.”

Aubameyang amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Man United, akifunga mabao matatu katika mechi nne alizokumbana na miamba hiyo ya Old Trafford.

Arsenal ilimpa mkataba mpya wa miaka mitatu wenye thamani ya Pauni 350,000 kwa wiki siku tatu baada ya mechi ya kwanza ya ligi kwenye ushindi dhidi ya Fulham. Na tangu hapo, alifunga mara moja kwenye Europa League dhidi ya Rapid Vienna huku akitoka kapa mechi sita za ligi.

Baadhi ya mashabiki wanamlaumu Mikel Arteta kwa ukame huo wa mabao ya Aubameyang kwamba amekuwa akimchezesha pembeni badala ya kumweka kati karibu na goli. Lakini, kocha huyo wa Arsenal, Arteta alisema baada ya kipigo kutoka kwa Leicester City kwamba kila mchezaji anapaswa kutimiza wajibu wake bila ya kujali anacheza wapi.