United kuanza na Chelsea Trafford Ligi Kuu England

Muktasari:

Mechi ya kwanza ya wapinzani wa jadi wa Jiji la Manchester, City na United itachezwa Desemba wakati pambano la marudiano litakuwa Machi.

LONDON, ENGLAND . WAZUNGU hawacheleweshi. Ratiba ya Ligi Kuu ya England imetoka jana Alhamisi na Manchester United na Chelsea zitakutana katika pambano la kwanza Agosti 11 Old Trafford ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Chelsea bila ya staa wake Eden Hazard aliyehamia Real Madrid.

Achilia pambano hilo ambalo litakuwa gumu kwa Kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye ataanza msimu wake wa kwanza kamili Manchester United, Tottenham nayo itaanza na mwanzo mgumu kwa kucheza na Manchester City na Arsenal katika mechi zake nne za mwanzo ugenini.

City ambayo itakuwa inasaka taji lake la tatu mfululizo England baada ya kutwaa ubingwa msimu ulioisha kwa tofauti ya pointi moja na itaanza ligi ikiwa na mechi za kawaida kwa kucheza dhidi ya West Ham, Spurs, Bournemouth, Brighton, Norwich na Watford.

Mambo yatakuwa matamu Mwezi Novemba ambapo Liverpool iliyoporwa ubingwa kimafia na Man City itakapowakaribisha wapinzani wao Anfield Novemba 9. Baadaye City itaialika Chelsea wiki mbili zijazo kabla ya kufunga mwezi kwa kucheza na Newcastle.

Mechi ya kwanza ya wapinzani wa jadi wa Jiji la Manchester, City na United itachezwa Desemba wakati pambano la marudiano litakuwa Machi.

Pambano la kwanza la ufunguzi wa kampeni hizi linatarajiwa kuchezwa Ijumaa wakati Liverpool itakapowakaribisha wageni Norwich Anfield. Na baada ya hapo Liverpool itacheza na Southampton ugenini kisha kuikaribisha Arsenal nyumbani.

Liverpoo na Manchester City zitarudiana Aprili 4 na pambano ambalo kwa kiasi fulani katika nyakati hizo linaweza kuamua mbio za ubingwa. Pambano la wapinzani wa jadi wa Merseyside kati ya Liverpool na Everton la kwanza litarajiwa kuchezwa Desemba Anfield wakati la pili linatazamiwa kuchezwa Goodison Park Machi.

Kwa mara ya kwanza baada ya misimu minane Ligi Kuu ya England itamkosa Eden Hazard aliyekwenda Real Madrid kwa dau la Pauni 150 milioni. Chelsea ambayo ilimaliza ya tatu msimu uliopita itayumbishwa na kukosekana kwake pamoja na pia kufungiwa kununua wachezaji.

Kocha Maurizio Sarri anaweza asiwe katika kiti chake katika ratiba hii wakati huu akihusishwa kurudi Italia na baada ya Chelsea kucheza na United katika mechi ya kwanza maisha yao hayatakuwa magumu sana. Itacheza dhidi ya Leicester City nyumbani kabla ya kucheza dhidi ya wageni wawili mfululizo, Norwich na Sheffield United.

Kwa upande wa Spurs ambayo ilishika nafasi ya nne katika msimamo uliopita itaanzia nyumbani dhidi ya Aston Villa kabla ya kucheza mechi ngumu mbili za ugenini dhidi ya Man City kisha nyumbani kwa Newcastle.

Wakati huohuo, Unai Emery akiwa katika msimu wa pili na Arsenal ataanza kuhukumiwa vilivyo na mashabiki wa timu yake, baada ya kuanza na Newcastle United anatazamiwa kurudi nyumbani kucheza na Burnley kabla ya kusafiri kwenda Anfield kucheza na Liverpool kisha kurudi nyumbani kucheza na Spurs. Mechi ya marudiano na Spurs inatazamiwa kuchezwa Aprili mwakani.

Ratiba ngumu zaidi kwa Unai itakuja Krismasi ambapo atakuwa nyumbani katika mechi mbili mfululizo. Dhidi ya Chelsea Desemba 28 kisha dhidi ya Manchester United Januari Mosi.

Wakati City, Liverpool, Manchester United, City, Spurs na Arsenal zikitazamiwa kuwania ubingwa na Top Four, Klabu za Norwich, Sheffield United na Aston Villa zilizopanda zitakuwa zinataka kufuata nyayo za Wolves kubakia Ligi Kuu.

Norwich City inatazamiwa kuwa katika mwanzo mgumu kwa kuanza kucheza na Liverpool ugenini kisha mechi mbili za nyumbani dhidi ya Newcastle na Chelsea kabla ya kwenda London kucheza na West Ham.

Sheffield United iliyorudi Ligi Kuu baada ya kupotea kwa miaka 12 haitaanza pabaya.

Itaanza kwa kucheza na Bournemouth ugenini kabla ya kurudi nyumbani na kucheza mechi mbili dhidi ya Crystal Palace na Leicester City.

Aston Villa baada ya kurudi katika Ligi Kuu itaanza kwa kucheza yake dhidi ya Spurs ugenini kabla ya kurudi nyumbani katika uwanja wao maarufu wa Villa Park kucharurana na Bournemouth kisha itacheza dhidi ya Everton.