JICHO LA MWEWE : Unapoyashangaa ya Aishi, Makambo na Bocco

Muktasari:

  • Kila mtu anasema lake kuhusu Makambo. Kuna taarifa ameuzwa kwa dau la Sh 230 milioni. Hapohapo kuna taarifa nyingine za kuchanganya zinaingia ndani yake. Mtu mmoja muhimu klabuni kasema ‘Makambo bado mali ya Yanga’.

MAGAZETI yameanza kuuza kwa kutumia habari za usajili. Ni kitu kinachofurahisha. Msimu wa mavuno kwa magazeti na wachezaji umewadia. Unasoma habari ambayo inakusikitisha halafu nyingine inakufurahisha na unacheka mpaka unatoa machozi.

Kwa mfano, nimesoma mahala. Kipa wetu namba moja nchini katika kikosi cha Taifa Stars, Aishi Manula amemaliza mkataba wake Simba. Nilisoma mahala amesaini mkataba mpya Simba. Nikasoma mahala tena kwamba Yanga wanamuhitaji kwa pesa nzuri tu.

Hapo hapo unajiuliza, mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, anakaribia kwenda kukipiga michuano ya mataifa ya Afrika pale Misri, kwanini asaini mkataba mpya Bongo? kwa uwezo wa Aishi si angejiweka sokoni Misri?

Katika Wikipedia nimezatama na kugundua kuwa Aishi ana umri wa miaka 23 tu. Wakati ndio huu. lakini mtu mmoja ameniambia hana mpango huo. Anasema anataka pesa ya haraka haraka hapahapa nchini.

Tanzania bado hakuna pesa nyingi za soka kama wachezaji wetu wanavyofikiri. Wanaweza kukusanya shilingi 100 milioni kwa sasa lakini kama wangekaza na kuvuka hatua moja mbele, basi kuna pesa nyingi zaidi ya hivi ambazo wanagombania katika usajili kwa sasa.

Wachezaji wa kulipwa wanapambana kwa kila namna waweze kuwa wachezaji huru huku wakiwa katika ubora wao kwa ajili ya kujiweka sokoni na kupata pesa nyingi zaidi. Tanzania, mchezaji bora anaamua kujiweka sokoni kwa timu mbili tu ambazo zinamlipa pesa kwa madafu. Huwa inatokea Tanzania tu. Kwingineko ambako wachezaji ni wapambanaji, hii inakuwa fursa. Hasa anapokaribia kucheza michuano mikubwa kama ya Afcon.

Unaachana na hili la Aishi unakutana na lile la Heritier Makambo wa Yanga. Nasikia ameuzwa kimyakimya kwenda klabu ya Horoya ya Guinea. Hii ni klabu tajiri. Tatizo suala la kuuzwa kwake limefanywa kama vile suala la mauzo ya bangi. Linaendeshwa chinichini na hakuna uwazi.

Kila mtu anasema lake kuhusu Makambo. Kuna taarifa ameuzwa kwa dau la Sh 230 milioni. Hapohapo kuna taarifa nyingine za kuchanganya zinaingia ndani yake. Mtu mmoja muhimu klabuni kasema ‘Makambo bado mali ya Yanga’.

Walimwengu waliwahi kusema ‘Samaki mkubwa anamla samaki mdogo’. Rais wa Real Madrid, Florentino Perez wakati akitangaza ubabe wa kumnunua Zinedine Zidane kutoka Juventus aliwahi kusema ‘Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani, inategemea ni kiasi gani cha pesa ulichonacho’.

Unaweza kumuuza Makambo kwa dau hilo, ukaenda nchi nyingine jirani kuionea klabu nyingine na kumnunua mshambuliaji kwa gharama za jumla ya Sh 100 milioni.

Wakati mwingine tunaogopa lawama kutoka kwa wanachama. Ndivyo tulivyo. Biashara ya Makambo inafanyika kama vile kuna mauzo ya bangi.

Ukiachana na habari za Aishi na Makambo unakutana na habari ya John Bocco. Nasikia Azam ilipambana kwelikweli kutaka kumrudisha klabuni kwao. Hapo ndipo unapowashangaa Azam. Hawajui wanachotaka katika klabu yao.

Miaka miwili iliyopita walidai wanataka kuachana na wachezaji wao wakongwe na kuanza upya. Waliachana na Aishi, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na John Bocco walioenda Simba. Nyakati zile nilijiuliza, hata kama unaachana na wachezaji hawa, kwanini waende kuiimarisha Simba?

Lakini muda wote ambapo Nyoni, Aishi, Kapombe na Bocco wanakuwa fiti, basi lazima waanze katika kikosi cha kwanza.

Unawaacha vipi wachezaji ambao wapo katika vilele vyao vya usakataji soka?Kwa Bocco, kilichoshangaza zaidi ni kwamba baada ya kuachana na yeye wakaamua kuwachukua kina Obrey Chirwa na Donald Ngoma.

Ukweli ni kwamba Bocco ana rekodi bora zaidi kuliko hao. Iweje waliachana naye na kuwachukua hao?

Leo wanataka kumrudisha tena Bocco ingawa tayari ameshasaini Simba. Walitaka kumrudisha kwa maana wameshabadili tena falsafa yao ya soka? Wamenyoosha mikono juu na kugundua mpira wa siku hizi unaendeshwa zaidi na wachezaji ambao wamekamilika uwanjani?

Zama za kujaribu kutumia makinda kama alivyofanya Arsene Wenger zimepitwa na wakati. Kwa timu yenye pesa kwanini iliingia mkenge wa kuachana na mchezaji kama Bocco ambaye hapana shaka ni mshambuliaji bora zaidi nchini kwa wanasoka wa Kitanzania wanaocheza ndani?