Unapenda ligi ya NBA? Imerudi rasmi

Muktasari:

Ligi hii ndio mchezo unaopendwa zaidi nchini Marekani kuliko soka na baadhi ya michezo mingine iliyopo katika taifa hilo lenye nguvu kubwa Duniani.

Dodoma. Hatimaye msimu mpya wa ligi ya kikapu nchini Marekani NBA (Regular Season) unatarajiwa kuanza usiku wa leo Jumanne nchini humo na alfajiri ya Jumatano kwa saa Afrika Mashariki.

Ligi hiyo inarejea ikiwa na taswira tofauti kwa baadhi ya kanuni zake kuboreshwa ili kunogesha zaidi ligi hiyo inayofuatiliwa zaidi kuliko ligi nyingine za Kikapu katika mataifa yote Duniani.

Ni msimu ambao wengi wanasubiri kujua nini kitatokea katika kanda zote mbili za Maashariki na Magharibi ambazo zina kitu kipya cha kutazamwa.

Ukanda wa Mashariki msimu huu kitakachotazamwa zaidi ni timu ipi kati ya Boston Celtics,Toronto Raptors, Miami Heat ama Philladelphia 76ers  itakayovunja utawala wa Clevaland Cavaliers iliyoondokewa na aliyekuwa nyota wake LeBron James.

Upande wa Magharibi ndipo kunatarajiwa kuwa na vita ya aina yake msimu huu kuliko Mashariki ambapo mbali na Houston Rockets waliokaribia kufika fainali msimu uliopita dhidi ya Golden State Warriors lakini kuongezeka kwa LeBron James katika timu ya Los Angeles Lakers kutaongeza msisimko zaidi.

Ni mara ya kwanza pia LeBron James atacheza ukanda wa Magharibi ambapo tangu aanze mchezo huo amechezea timu 2 pekee za Clevaland Cavaliers,Miami Heat kabla ya kurudi tena Cavaliers zote za ukanda wa Mashariki na katikati ya mwaka huu kuelekea Magharibi kuichezea Los Angeles Lakers.

Ufunguzi wa ligi hiyo utafunguliwa na mchezo mmoja kila ukanda ambapo mapema Saa 9 alfajiri mabingwa wa kihistoria Boston Celtics watacheza dhidi ya Philladelphia 76ers wakati ukanda wa Magharibi vita itaanzishwa na bingwa mtetezi Golden State Warriors dhidi ya Oklahoma City Thunder mchezo utakaoanza saa 11:30 alfajiri.