Unamtaka Umtiti? Lete Pauni 44milioni

Muktasari:

Kutokana na athari za kiuchumi katika klabu nyingi zilizotokana na janga la virusi vya corona, inadaiwa kuwa Umtiti ataruhusiwa kuondoka Barcelona kwa Pauni 44 milioni.

BARCELONA, HISPANIA . BARCELONA wameripotiwa kujiandaa kumuuza beki wao Mfaransa Samuel Umtiti kwa ada ya uhamisho ya Pauni 44 milioni katika dirisha lijalo la uhamisho la majira ya kiangazi.

Ingawa Umtiti amecheza mechi 114 tangu alipoondoka Lyon mwaka 2016, beki huyo wa kati amekuwa siku za hivi karibuni nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha au akijikuta akitupwa benchi la wachezaji wa akiba.

Huku beki huyo mwenye umri wa miaka 26 akiendelea kutajwa kama mmoja wa mabeki bora barani Ulaya, mwandishi wa habari wa Italia, Nicola Schira, amedokeza kwamba miamba hiyo ya Catalunya iko tayari kupokea mkwanja kwa klabu yoyote inayohitaji huduma ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia.

Kutokana na athari za kiuchumi katika klabu nyingi zilizotokana na janga la virusi vya corona, inadaiwa kuwa Umtiti ataruhusiwa kuondoka Barcelona kwa Pauni 44 milioni.

Manchester United, Arsenal na Chelsea zote zimekuwa zikihusishwa na mipango cha kutaka saini ya beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa katika miezi ya hivi karibuni.

Umtiti bado ana miaka mitatu imebaki katika mkataba wake, jambo linaloipa Barca nguvu ya kupanga bei wanayoitaka.