Umesikia hii ya kuhusu Salah?

Muktasari:

  • Hispania ndiko walikoanza chokochoko kwamba Mo Salah anataka kuondoka zake licha ya kuwa na msimu bora kabisa huko Liverpool mwaka jana huku msimu huu akiendelea kutamba katika kuisogeza timu kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.

LIVERPOOL, ENGLAND.LISEMWALO ni kwamba supastaa Mohamed Salah hana uhusiano mtamu sana na kocha wake Jurgen Klopp huko Liverpool, ndivyo zinavyodai taarifa za kutoka Ufaransa.

Kumekuwa na madai kwamba staa huyo wa kimataifa wa Misri amekuwa akihitaji kuhama na hilo ndilo linalosemwa kwamba chanzo cha wawili hao kutokuwa na uhusiano mzuri.

Hispania ndiko walikoanza chokochoko kwamba Mo Salah anataka kuondoka zake licha ya kuwa na msimu bora kabisa huko Liverpool mwaka jana huku msimu huu akiendelea kutamba katika kuisogeza timu kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.

Taarifa hizo ziliwashtua mashabiki wa Liverpool, ambao wamekuwa na mapenzi makubwa na mchezaji huyo tangu alipojiunga na timu yao mwaka 2017.

Wakala wake Mo Salah alilishambulia gazeti la AS la Hispania akidai kuripoti mambo ya uongo katika taarifa yao ya awali kwamba Mo Salah hana uhusiano mzuri na kocha wake huko Anfield. Lakini, sasa licha ya kukanusha huko, taarifa nyingine za kutoka Ufaransa zimekinukuu chanzo kimoja kilichosema: “Mo Salah hana maelewano mazuri tena na bosi wake Jurgen Klopp.”

Jambo hilo linaonekana kuwatibua mashabiki wa Liverpool na kuamua kutumia kurasa zao za Twitter kuelekezea hasira zao huku mmoja akiandika: “Acheni kuendeleza huo ujinga wenu”, huku mwingine akiandika: “Salah ataendelea kubaki kuwa mchezaji wa Liverpool mpende msipende.” Mashabiki wengine wanaamini kwamba Real Madrid na Barcelona zimekuwa zikitumia vyombo vya habari kuwavuruga wachezaji.