Umesikia? Eti Van De Beek angeitosa Man Utd

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO wa Kidach, Donny van de Beek ameambiwa k ni heri angowamea Manchester United na kubaki zake Ajax.

Hayo ni maneno ya Mdachi mwenzake, Marco van Basten - ambaye amekosoa namna Man United inavyomfanyia kiungo huyo iliyemsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Real Madrid walionyesha dhamira pia ya kumsajili staa huyo kabla ya kukubali kwenda Old Trafford kwa ada ya Pauni 40 milioni mwezi uliopita.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amekuwa hamchezeshi sana Van de Beek, akitokea benchi kwenye mechi nne za Ligi Kuu England.

Jumamosi iliyopita kwenye sare ya 0-0 uwanjani Old Trafford katika ligi dhidi ya Chelsea, Mdachi huyo aliachwa tu benchi mechi yote huku kocha Solskjaer akiwaingiza Mason Greenwood, Edinson Cavani na Paul Pogba.

Van Basten alisema: “Donny asingeenda kabisa Manchester United.

“Unapokuwa mchezaji mzuri unataka ucheze kila wiki. Ni mbaya sana kwa mchezaji kama Donny kucheza mechi sita au saba tu msimu huu. Hilo linakuharibia kabisa mwenendo wa soka lako. Donny angebaki tu kusubiri klabu nyingine bora zaidi.” Wakati hilo likizungumzwa, beki wa zamani wa Man United, Patrice Evra alihoji kama timu hiyo inahitaji huduma ya mkali huyo.

“Hebu tumzungumzie Van de Beek. Sina baya na huyu dogo, lakini kwanini tulimsajili? Amekuwa akitazama mechi zetu zote akiwa kwenye benchi. Hiyo ina maana hatumhitaji, huo ndio ukweli,” alisema Evra.