Umesikia... Winga wa UD Songo kutua Yanga

Muktasari:

Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kutoka Maputo, kiongozi mmoja wa Yanga (jina tunalo) na kuzungumza naye akimtaka awatumie pasi yake ili kuweza kufanyiwa mchakato wa kutumiwa tiketi kuwahi mapema kabla hata dirisha dogo halijachanganya baada ya kufunguliwa Desembe 16.

UNAMKUMBUKA yule winga matata aliyekuwa akisepa na kijiji katika mechi iliyowang’oa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi yas UD Songo? Sasa unaambiwa jamaa anataka kutua Yanga licha ya awali mabosi wa Msimbazi walimpigia hesabu wakiamini ataziba nafasi ya Emmanuel Okwi.

Winga huyo kama umemsahau ndiye aliyeifunga bao la mapema Simba kwenye Uwanja wa Taifa na kuwatibulia safari yao ya msimu huu katika michuano ya CAF na mwishowe kuotesha kibarua cha Kocha Patrick Aussems.

Luís Jose Miquissone, ambaye mbali ya kuonyesha mpira mkubwa katika mechi zote mbili dhidi ya Simba, aliweza kuifungia timu yake bao la kwanza katika mechi ya marudiano iliyochezwa Uwanja wa Taifa na Simba kulisawazisha na kuwang’oa kwa kuwapa faida ya bao la ugenini UD Songo.

Mabosi wa Yanga wamekuwa wakifanya siri kubwa juu ya kumleta winga huyo, lakini Mwanaspoti limenasa mkanda mzima wa mpango huo, huku mchezaji huyo akikiri kupigiwa simu na kuzungumza na mmoja wa vibosile wa Yanga ili wamlete dirisha dogo la usajili.

Uongozi wa Yanga umeelezwa umeanza mipango ya kuisuka timu hiyo na hesabu zao za kwanza zimedondoka kwa Misquissone, ambaye alipendekezwa mapema mwaka huu na mabosi wa Simba kumvuta Msimbazi kuziba pengo la Okwi kabla ya kubanwa na mkataba.

Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kutoka Maputo, kiongozi mmoja wa Yanga (jina tunalo) na kuzungumza naye akimtaka awatumie pasi yake ili kuweza kufanyiwa mchakato wa kutumiwa tiketi kuwahi mapema kabla hata dirisha dogo halijachanganya baada ya kufunguliwa Desembe 16.

Misquissone alikiri ni kweli alipigiwa simu na viongozi watatu wa Yanga, ila akamtaja mmoja mbali na kuongea Kiingereza lakini walikuwa wakielewana zaidi kwa maana anajua vizuri kireno na kuelewana naye.

“Maongezi yetu yalikuwa mazuri kati ya viongozi hao wote watatu ambao walinipigia simu na hatua ambayo tumefikia wakati huu ni kusubiri kutumiwa tiketi ya kuja huko Tanzania kwani mpaka Passport yangu nimewatumia tayari,” alisema.

“Nina mkataba na Mamelodi Sandowns ya Afrika Kusini iliyonirudisha kwa mkopo UD Songo, lakini siku si nyingi naenda kuvunja mkataba wangu na kuwa mchezaji huru ili niweze kusaini popote,” alisema Miquissone.

“Nimemaliza majukumu yangu ya UD Songo kwani Ligi ya Msumbuiji imemalizika jana (juzi) Jumatano kwa maana hiyo nipo huru kwenda timu yoyote ili kuzungumza nayo na kama tutakubaliana naweza kusaini hapo,” alisema.

“Kuhusu mkataba na Mamelodi sina wasiwasi kwangu kwani suala la kuvunja linawezekana kutokana kuna mambo hayakuwa yanakwenda sawa,” aliongezea Miquissone.

Mmoja wa vigogo waliopo kwenye Kamati ya usajili wa Yanga aliliambia Mwanaspoti, kila kitu kuhusu usajili utatangazwa, hivyo kuanza kumzungumzia winga huyo kwake ni vigumu.

Nyota huyo Miquissone, alizaliwa Msumbiji Julai 25, 1995, akimudu nafasi ya kiungo mshambuliaji anayetokea pembeni au kati na klabu yake ya kwanza kumtambulisha na UD Songo kabla ya kunyakuliwa na Mamelodi ambayo imekuwa ikimtoa kwa mkopo kwa timu tofauti zikiwamo Chippa United na Royal Eagles zote za Afrika Kusini kabla ya msimu kurejeshwa UD Songo.

Rekodi zinaonyesha Miquissone, ameanza kucheza timu ya taifa ya Msumbiji chini ya miaka 20 mwaka 2013 kabla ya kuitwa timu ya wakubwa mwaka 2015 akiichezea mpaka leo akiwa amecheza mechi 27 na kufunga mabao tisa.

Aidha katika hatua nyingine, Yanga ipo hatua ya mwisho kabla ya kumalizana na straika Tariq Seif aliyekuwa Biashara.

Nyota huyo aliyewahi kutamba Stand United, alipokewa jana mchana na Katibu Mkuu wa Yanga, Dk David Ruhago tayari kwa mazungumzo yanayaoelezwa huenda yakakamilika leo Ijumaa kabla ya kusaini mkataba.