Ulinzi mkali Yanga, Mbao hofu tupu

Muktasari:

  • Mchezo huo utakuwa na upinzani mkali kwani Mbao FC wanataka kuendeleza rekodi yao ya kushinda huku Yanga wakiwa na hasira ya kipigo cha bao 1-0 kutoka Simba na kutaka kufuta uteja uwanjani hapo.

MWANZA .VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wametua jijini hapa jana asubuhi tayari kuwakabili wenyeji wao Mbao FC huku Yanga wenyewe wakipania kuvunja mwiko kwenye mchezo utakaopigwa kesho Jumatano Uwanja wa CCM Kirumba.

Yanga ilitua jijini hapa saa 1:30 asubuhi ikiwa na kikosi cha nyota 20 sambamba na benchi la ufundi huku mamia ya mashabiki wakifurika kuwapokea kwa shangwe.

Mashabiki hao wakiongozwa na viongozi wao wa matawi walifika uwanja wa Ndege wa Mwanza huku Kocha Mwinyi Zahera pamoja na kipa Claus Kindoki wakishangiliwa.

Wakati Yanga wakitua, wenzao Mbao FC walikuwa wakijifua Uwanja wa Kirumba huku wakiwa hawana presha ya ujio wa wapinzani wao.

Hata hivyo, Yanga haijawahi kupata ushindi wowote uwanja wa Kirumba katika mechi tatu walizocheza na Mbao FC zote wamekutana na kichapo.

Mchezo huo utakuwa na upinzani mkali kwani Mbao FC wanataka kuendeleza rekodi yao ya kushinda huku Yanga wakiwa na hasira ya kipigo cha bao 1-0 kutoka Simba na kutaka kufuta uteja uwanjani hapo.

Baada ya timu hiyo kuwasili, jana jioni walianza mazoezi kweye uwanja wa Nyamagana huku ulinzi mkali ukiimarishwa na kutoruhusu mashabiki kushuhudia mbinu ambazo Zahera alikuwa akizitoa kwa wachezaji wake.

Pamoja na ulinzi huo, mashabiki walijipenyeza na kushuhudia sehemu ya mazoezi ya timu hiyo.

Zahera afunguka

Zahera ambaye anajua fika rekodi tamu ya Mbao FC wakiwa uwanja wa Kirumba, alisema mambo ya rekodi ni ya zamani na sasa wamekuja kuchukua pointi tatu.

Alisema kinachompa nguvu ya kutamba kuvunja rekodi na kuondoa uteja ni kutokana na kikosi chake alichokuja nacho ambacho amedai kina ari na morari kubwa. Mkongo huyo alifafanua kuwa hata kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Simba ni makosa madogo ambayo anaamini hayatajitokeza badala yake ni ushindi tu.

‘‘Hatuchezi kwa rekodi hayo ni mambo ya zamani, tumekuja kupambana kuhakikisha tunashinda, timu iko fiti na hakuna mchezaji mwenye majeruhi ,’’ alisema Zahera.

Benitez presha juu

Wakati Yanga wakiwasili kwa mbwembwe, Kocha wa Mbao, Ally Bushiri ‘Benitez’ alikuwa bize kuwanoa wachezaji wake huku kukiwa na mvua.

Katika mazoezi hayo Benitez alionekana kuikomalia zaidi safu ya ushambuliaji ambapo aliwapanga Raphael Siame, Evarigustus Mjwahuki, Rajesh Kotecha na Pastory Atanas ambao muda wote walikuwa wakipiga mashuti.

“Tutaingia kwa tahadhari kubwa kwenye huu mchezo tunajua Yanga wana hasira ya kipigo kutoka kwa Simba, tumejipanga kuwakabili kwani, tunataka tuendeleze rekodi yetu,” alisema Benitez.

Makambo ahofiwa

Beki wa kati wa Mbao FC, Erick Murilo, amesema kama kuna mchezaji tishio ndani ya Yanga basi ni Heriettie Makambo akitoa sababu kuwa ni mchezaji asiyetulia eneo moja hivyo inakuwa ngumu kumkaba.

“Tunawaheshimu Yanga ni wazuri na wazoefu katika soka, lakini tupo tayari kwa ushindani na dakika 90 ndio zitaamua,” alisema Murilo.