Breaking News
 

Maskini uwanja wa Nyamagana ndiyo basi tena

Saturday January 13 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Ukuta wa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza umebomolewa leo, Jumamosi kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.
Ubomoaji wa ukuta huo ni utekelezaji bomoabomoa wa nyumba au taasisi zote zilizojengwa ndani ya mita 15 hadi 30 ya njia ya reli unaofanywa na Kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (Rahco).
Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza wamiliki wa uwanja huo uliowekwa nyasi za bandia hivi karibuni, Kiomoni Kibamba alisema mbali na Nyamagana, ubomoaji huo utaathiri maeneo mbalimbali ikiwamo nyumba na taasisi.
 “Taasisi zitakazoathirika ni pamoja na ukuta wa uwanja wa mpira Nyamagana, ukuta wa mamlaka ya bandari(TPA), kiwanda cha Samaki cha Vicky Fish na taasisi zingine yakiwemo makanisa na nyumba za kawaida”alisema Kibamba.
 Akizungumzia ubomoaji huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA),Leonard Malongo alisema kuwa huo ni utaratibu ambao ulitangazwa mapema, hivyo wanalipokea kama lilivyotokea.
 Alisema wao MZFA, wanawaomba wamiliki wa uwanja huo, Halmashauri kuhakikisha wanakarabati haraka ukuta huo ili kulinda mali zilizomo ndani ya uwanja na kutozuia shughuli za michezo.
 “Sisi tunalipokea kawaida, ni utaratibu, lakini niombe Halmashauri ya Jiji waharakishe kukarabati huu ukuta kwa sababu kuna mali mle ndani, lakini gharama iliyotumika ni kubwa na tunautegemea sana huu uwanja,” alisema Malongo.
Wadau wa soka jijini hapa, Ahmad Hussein na Juma Mohamed walisema kuwa zoezi hilo ni sahihi kwani kila kitu kina utaratibu wake.
“Ni sahihi kwa sababu ukisema uwanja usiingiliwe unakuwa umependelea pande moja, makanisa, misikiti, ofisi za watu zivunjwe iweje uwanja? Lazima sheria iguse pote,”alisema Hussein.
Hata hivyo, baada ya ubomoaji huo, viongozi wa MZFA walikuwa wakihangaika kutafuta maturubai na mavero kufunika eneo hilo,ili watazamaji wa mechi ya Toto Africans na Oljoro wasiingie uwanjani bila kulipa viingilio.