Ukuta Stars wamkosha Amunike

Muktasari:

Kesho Jumapili, Taifa Stars itacheza mchezo wa pili na wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Zimbwabwe kwa ajili ya kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ilikopangwa kundi C pamoja na Kenya, Algeria na Senegal


NIDHAMU  ya kujilinda iliyoonyesha na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Misri juzi Alhamisi imemkosha kocha Emmanuel Amunike aliyetamba itaibeba timu hiyo kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Borg El Arab huko Alexandria Misri kama sehemu ya kipimo cha kujiandaa na fainali za AFCON, Stars ilicheza vizuri safu ya ulinzi ambayo haikufanya makosa ya mara kwa mara kama ilivyozoeleka hapo awali ingawa ilipoteza kwa bao 1-0.
Stars ilitumia muda wa takribani robo tatu ya dakika 90 za  mechi hiyo katika kujilinda na dakika 15 za mwisho angalau ilionekana kufunguka na kujaribu kupeleka mashambulizi kwa Misri ingawa haikuweza kufunga bao lolote.
Amunike ameonesha kufurahishwa na hilo na kudai kuwa kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake ni ishara tosha kwamba wameimarika kwa kiasi kikubwa kuelekea mechi za AFCON.
"Tulicheza kwa ajili ya kuziba mianya dhidi ya Misri na tulifanikiwa. Lengo letu ni kuimarika kadri tuwezavyo na pia kuboresha viwango vyetu.
"Ni kweli tunacheza kundi gumu lakini tutafanya kadri tuwezavyo tuweze kufuzu raundi ya pili," alisema Amunike akihojiwa na mtandao wa kingfut.com
Kwenye fainali za AFCON, Tanzania itafungua dimba kwa kucheza na Senegal, Juni 23 na baada ya hapo, Juni 27 itakwaana na Kenya na mchezo wa mwisho itapepetana na Algeria, Julai Mosi.