Ukuta Stand United unachomesha kinoma

Saturday November 10 2018

 

By CHARITY JAMES

Dar es Salaam. Stand United 'Chama la Wana' ndiyo timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi 21, katika Ligi Kuu Bara, jambo linaloonyesha udhaifu wa ngome yao ya ulinzi iliyo chini ya Mrundi Bigirimana Ramadhani.

Si msimamo wa Ligi Kuu pekee kuoonyesha udhaifu wa mabeki wa Chama la Wana, bali kocha wao msaidizi, Athuman Bilali 'Bilo' amethibitisha hilo na kusisitiza wanalifanyia kazi na watasajili wachezaji wengine katika dirisha dogo.

Stand ambayo katika safu hiyo ya ulinzi inaongozwa na Ahmed Kajigili, Erick Mulilo, Babu Ally, Erick Ndilioba na Bigirimana Nassoro wamekuwa wakifanya makosa yanayofanana.

"Ni kweli safu yetu ya ulinzi imeonekana kuwa na tatizo sehemu hiyo tunatakiwa kuongoza kwa idadi ya kufunga mabao lakini kwetu imekuwa ni kinyume, tunaruhusu mabao mengi ya kufungwa," alisema Bilo.

Stand United imecheza michezo 14, imeshinda minne, imetoka sare miwili, imepoteza minane. Imefunga mabao 14, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21, na kufanikiwa kuvuna pointi 14.

Advertisement