Ukata wamkimbiza Mfaransa African Lyon

Muktasari:

Mshambuliaji Mfaransa wa African Lyon, Victo Da Costa ameondoka nchini kwa madai ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mshahara wa miezi miwili.

Mbali na Da Costa, pia kocha wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Soccoia Lionel amerejea Ufaransa

Dar es Salaam. Kocha wa African Lyon inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Soccoia Lionel na mshambuliaji Mbrazil Victor Da Costa wametimka katika kikosi hicho.

Lionel na Da Costa ambao ni raia wa Ufaransa, walijiunga na African Lyon, lakini wamedumu muda mfupi kabla ya juzi kurejea nchini mwao.

Akizungumza kwa simu kutoka Paris jana, Da Costa alidai ameshindwa kuendelea na mkataba African Lyon kutokana na mazingira magumu ya maisha.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na African Lyon akitokea Magni ya Iceland, amefunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United.

“Niko Paris nimeamua kurudi nyumbani kwa sababu maisha African Lyon yamenishinda. Sijawahi kuona klabu ikishindwa kumlipa mshahara kwa siku 60,” alisema Da Costa.

Alisema alikuwa na malengo ya kutoa mchango African Lyon kwa kutumia kipaji chake, lakini kitendo cha kuishi miezi miwili mshahara kilimkatisha tama.

"Kocha naye ameondoka kutokana na mazingira magumu ya kufanya kazi, hivi tunavyozungumza (jana mchana) tuko Paris," alisema Da Costa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ alidai kocha na mchezaji huyo wamerejea Ufaransa kwa mapumziko.

"Da Costa na kocha hawapo, lakini wamekwenda likizo, kwani nyie hamuoni ligi imesimama, ikianza watarudi," alisema Zamunda.

Hata hivyo, Zamunda aliweka ngumu kuzumzia kutolipwa mshahara kwa miezi miwili akidai ni mambo binafsi  baina ya mwajiri na mwajiriwa.