Ukata Yanga umewabeba

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota hao ambao kwa sasa wapo Yanga kwa ajili ya ukata na wasipopiga mahesabu ya kuangalia mbele wanaweza wakajikuta wanafanyiwa ‘sapraizi’ siku Wanajangwani wakitengamaa kiuchumi.

SI jambo la kificho Yanga kuwa kwenye wakati mgumu kiuchumi kwa sasa, hilo ndio sababu ya mlundikano wa wachezaji wasio na sifa ya kuvaa uzi wa kijani na njano pale Jangwani.

Yanga ni taasisi kubwa ya kushindana kimataifa na usajili wake unatakiwa uwe wa wachezaji wa viwango vya juu vitakavyoendana na thamani ya klabu hiyo.

Ukata ulioikumba klabu hiyo baada ya aliyekuwa mwenyekiti wao Yusuph Manji kupata matatizo, umefanya benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo kuvumilia kukaa na badhi ya wachezaji wasio na sifa ya kuvaa uzi wa njano na kijani.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota hao ambao kwa sasa wapo Yanga kwa ajili ya ukata na wasipopiga mahesabu ya kuangalia mbele wanaweza wakajikuta wanafanyiwa ‘sapraizi’ siku Wanajangwani wakitengamaa kiuchumi.

KLAUS NKINZI KINDOKI

Kindoni raia wa DRC ya Kongo, alitarajiwa kuibua ushindani dhidi ya kipa Beno Kakolanya, ili kuhakikisha ngome ya ulinzi ya Yanga inakuwa imara kama ilivyokuwa kwa Ally Mustapha ‘Bartez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’, ila haijawa hivyo mpaka sasa.

Usajili wa Kindoki ulitikisa mwanzoni mwa msimu huu wa 2018/19 na matarajio ya mashabiki yalikuwa ni kushuhudia uhodari wake katika kupangua hatari za washambuliaji wa upinzani, alishindwa kufanya hivyo kwa baadhi ya mechi alizodaka na kumpa ujiko Kakolanya kuaminiwa zaidi na mashabiki.

PATO NGONYANI

Si mchezaji anayepangwa ndani ya kikosi cha Kwanza, tangu akiwa chini ya kocha Hans Pluijm (aliyepo Azam FC), George Lwandamina (karudi Zesco) na bado hapati nafasi mbele ya kocha Mwinyi Zahera, hilo linadhihirisha salama yake ni ukata ulioikumba klabu hiyo.

JUMA MAHADHI

Licha ya kupewa nafasi na makocha mbalimbali waliopita kwa nyakati tofauti Yanga, alishindwa kuonyesha na hata alipoondoka Saimon Msuva kwenda Difaa El Jadida ya Morocco, aliyekuwa anamuweka benchi, alitarajiwa kuziba nafasi yake, lakini haijawa hivyo.

EMMANUEL MARTIN

Angalau chini ya George Lwandamina, Martin alikuwa anapata nafasi ndani ya kikosi cha kwanza na kipindi hicho kikosi kilikuwa na majeruhi wengi na pia ilikuwa kwenye ukata, msimu wa 2018/19 hali ni mbaya kwake, hajafanikiwa kupangwa mechi hata moja zaidi ya kucheza za kirafiki.

ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’

Yanga ya Yusuph Manji (aliyekuwa mwenyekiti), ilisajili beki visiki na walionyesha uwezo wa hali ya juu, kama Mbuyu Twite, Vincent Bossou lakini mambo yalipoanza kuyumba, viongozi walikuwa wanaumiza vichwa namna ya kuunda kikosi, wakapatikana kina Ninja, uchumi ukija kukaa sawa basi inaweza kuwa ngumu beki huyu kupata namba.

RAPHAEL DAUD

Alipokuwa Mbeya City, nuru yake iling’ara kiasi kwamba Simba, Azam zilihitaji huduma yake, Yanga ikawapiga bao na kufanikisha saini yake, huenda kiwango anachokionyesha kwa sasa kinatokana na hali nzima ya timu lasivyo kama amejibweteka Yanga ikiwa vizuri kiuchumi ni kati ya majina yanayoweza kufyekwa.

MATHEO ANTHONY

Ni kama yupo Yanga kwa mazoea kwani ni kati ya wachezaji ambao wamebahatika kupewa nafasi na makocha ambao wamewahi kukinoa kikosi hicho, kiwango cha Matheo kimekuwa hakionyeshi ushindani dhidi ya mastraika wanaokuwepo ndani ya kikosi hicho ni rahisi sana klabu hiyo ikitengemaa kiuchumi jina lake kukatwa.

JAFARY MOHAMMED

Tangu ajiunge na Yanga akitokea Majimaji ya Songea, Jafary hajawa na nafasi kubwa mbele ya kocha Mwinyi Zahera na usajili wake ulifanyika klabu hiyo ikiwa imeyumba kiuchumi.

HERITIER MAKAMBO

Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2018/19 una mzunguko mrefu badala ya mechi 30 zitakuwa 38, hilo linampa nafasi Makambo kuongeza juhudi ili kuonyesha kile ambacho Yanga walikitarajia kuziba pengo la Obrey Chirwa ambaye kwa sasa yupo Azam FC.

MRISHO NGASSA

Ngassa wa miaka mitano nyuma sio huyu wa sasa ni kweli amefunga baadhi ya mechi alizopangwa, lakini kwa Yanga ya ushindani kasi yake imepungua na ukata ndio ulifanya aweze kurejea kirahisi ndani ya kikosi hicho.

Wapo wachezaji ambao ni chipukizi na baadhi walipandisha kutoka Simba B kama Yusuf Mhilu, Yohana Mkomola na Ramadhan Kabwili walitoka Serengeti Boys, wanapaswa kuonyesha hawajaridhika badala yake kupitia Yanga iwauze nje.