Ujiko wa Jhikoman anavyopewa Diamond Platinumz kienyeji

Muktasari:

Ni kweli kwamba Jhiko alifanya na Peetah, wakati Diamond aliishirikisha bendi yote, lakini ukweli haupingiki kwamba Peetah ni staa wa Morgan Heritage.

MEI 2015, moja ya alama za muziki wa Reggae nchini, Jhiko Manyika ‘Jhikoman’, aliachia dude lenye jina “Afrika Arise”. Ndani ya ngoma hiyo ameshirikishwa Peetah Morgan wa kundi la Morgan Heritage.
Septemba 2017, Diamond Platnumz, aliuweka hadharani wimbo wake “Hallelujah “, kundi la Morgan Heritage lilihusika vema kabisa. Ukipiga hesabu, hapo kuna tofauti ya miaka miwili, miezi minne na ushee.
Morgan Heritage ni akina nani? Jawabu ni kwamba hawa ni nyota wa Reggae nchini Marekani lakini asili yao ni Jamaica. Ni watoto wa Denroy Morgan ambaye alikuwa mtu mkubwa sana katika Reggae, nyakati za uhai wake.
Watoto watano wa Denroy; Peetah, Una Morgan, Roy Morgan ‘Gramps’, Nakhamyah Morgan ‘Lukes’ na Memmalatel Morgan ‘Mr Mojo’, waliunda bendi yao mwaka 1994. Jina la bendi “Morgan Heritage “, yaani Urithi wa Morgan, ni kielelezo cha kumuenzi mzee wao.
Baada ya muhtasari, sasa tupunguze aya, tuelekee kwenye somo la leo. Ni kwamba ujiko ambao Jhikoman anaustahili kwa kuwa wa kwanza kufanya kazi na Peetah Morgan, anapewa Diamond Platnumz. Imekuwa ikitajwa mara nyingi kuwa Diamond ndiye wa kwanza kufanya kazi na Morgan Heritage, badala ya Jhiko.
Ni kweli kwamba Jhiko alifanya na Peetah, wakati Diamond aliishirikisha bendi yote, lakini ukweli haupingiki kwamba Peetah ni staa wa Morgan Heritage. Kwa mantiki hiyo, ladha ya Morgan Heritage, ilianza kusikika ndani ya kazi ya Tanzania kupitia kwa Jhiko na si kwa Diamond.
Ujiko huu anaostahili Jhiko lakini unakwenda kwa Diamond Platnumz, unapokelewa vipi na Jhiko mwenyewe?
JHIKOMAN: Inasikitisha. Inaonekana fani ya habari imevamiwa na watu ambao hawana misingi. Mtu badala ya kufanya utafiti ili aongee mambo kwa usahihi, yeye anazungumza ya kwake, matokeo yake anapotosha.
SWALI: Huoni labda wimbo wako hukuufanyia promosheni ya kutosha, kwa hiyo haufahamiki vizuri ndiyo maana Diamond anatajwa zaidi kupitia Hallelujah, kuliko wewe na Afrika Arise?
JHIKOMAN: Hiyo siyo sawa. Wimbo niliufanyia promosheni. Nilizunguka karibu vituo vyote kuutambulisha. Afrika Arise ipo YouTube yangu Mei 8, 2015. Ukiachia mbali hayo, wanahabari wanapaswa kuwa mbele ili kuusema ukweli. Wanahabari kuwa nyuma ni tatizo. Hili la kumpa sifa Diamond kuwa mwanamuziki wa kwanza Tanzania kufanya kazi na Morgan Heritage linaonesha jinsi baadhi ya wanahabari wetu walivyo nyuma.
SWALI: Je, unakubali kuwa Hallelujah wa Diamond umewatambulisha vizuri zaidi Morgan Heritage kuliko Afrika Arise?
JHIKOMAN: Kwa kiasi fulani naweza kukubali.
SWALI: Unadhani ni kwa nini wimbo wako haukuwa na nguvu kubwa ya kuwatambulisha Morgan Heritage kuliko Hallelujah wa Diamond?
JHIKOMAN: Kuna kipindi tu tunapitia ambacho si kizuri. Hata hivyo kuna kizazi kinakuja, chenyewe kitaupokea muziki mzuri. Utaona sasa hivi tunautumia muziki kufundishia zaidi. Najua muda ujao thamani ya muziki wetu itazingatiwa na biashara itafanyika.
Sasa hivi biashara ya muziki na burudani kwa jumla si nzuri. Hivyo na muziki ambao naufanya ni wa kuelimisha zaidi.
SWALI: Unaposema unautumia muziki kufundishia una maanisha nini?
JHIKOMAN: Mimi ni mwalimu wa sanaa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo. Vilevile nina darasa lingine kwenye ofisi yangu binafsi ya Afrikabisa. Naamini juhudi hizi zitaipa sanaa ya Tanzania thamani inayostahili siku za usoni.
SWALI: Unaizungumzia vipi Bongo Fleva na wasanii wa Bongo Fleva?
JHIKOMAN: Nawapongeza sana wasanii wa Bongo Fleva kwa sababu kazi wanayofanya ni kwa kutumia vipaji vyao tu. Hawajasoma sanaa na hawana elimu yoyote, kwa hiyo wanajitahidi sana.
SWALI: Unadhani Bongo Fleva inastahili kutawala soko la muziki Tanzania kama ilivyo sasa.
JHIKOMAN: Hapana. Ni upepo tu ndiyo unafanya Bongo Fleva uonekane upo juu. Siku zinakuja muziki mzuri utashika hatamu.
SWALI: Unadhani Reggae inakufa?
JHIKOMAN: Reggae haijafa na haitakufa. Reggae ni muziki mkubwa duniani. Reggae ni maisha. Kwa hiyo Reggae itaendelea kuwepo kwa sababu maisha yanaendelea.
SWALI: Nauliza kwa Tanzania, Reggae inakufa?
JHIKOMAN: Reggae haiwezi kufa Tanzania. Inacheleweshwa tu. Muda unakuja Reggae itastawi. Reggae ni muziki wenye nguvu kubwa.
SWALI: Kwa nini Reggae inasinzia? Ninyi kama wanamuziki wa Reggae mnashindwa kuutetea muziki wenu?
JHIKOMAN: Mfumo wa biashara ya muziki upo kama aina nyingine za biashara. Lazima kuwepo na matangazo. Muziki wa Reggae haupati nafasi kwenye vyombo vya habari ndiyo maana hauonekani. Ila Reggae ipo. Na itaendelea kuwepo. Siku ikianza kupewa nafasi katika vyombo vya habari, utaona nguvu yake.
SWALI: Tuambie muziki wako. Kuna kazi mpya au unakaribia kutoa kitu kipya?
JHIKOMAN: Nina EP mpya inaitwa Safari ya Gitaa Baridi. Ina nyimbo sita. Hiyo ndiyo kazi yangu mpya.
Ufafanuzi; EP (extended playlist), unaweza kuita albamu, lakini ujazo wa nyimbo unakuwa mdogo. Kwa wastani EP huwa na ujazo wa nusu ya albamu.
SWALI: Kwa nini EP yako inaitwa Safari ya Gitaa Baridi?
JHIKOMAN: Ni kwa sababu nimefanya, acoustic guitar, yaani muziki ambao naweza kufanya shoo popote nikiwa na gitaa langu tu.
SWALI: Safari ya Gitaa Baridi ni Reggae peke yake au umechanganya na mahadhi mengine?
JHIKOMAN: Safari ya Gitaa Baridi ni mkusanyiko wa ladha za Kiafrika hasa Tanzania. Vilevile kuna vionjo vya Reggae. Nimeshirikiana na bendi yangu ya Afrikabisa, vilevile walimu na wanafunzi wa Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.
SWALI: Nyimbo za Safari ya Gitaa Baridi ujumbe wake mahsusi ni nini? Mapenzi, harakati, siasa au burudani?
JHIKOMAN: Safari ya Gitaa Baridi nimeimba ujumbe unaogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania.