Ujenzi reli ya umeme (SGR) wamwibua Babu Tale, asema Wabongo wanaushamba

Muktasari:

Meneja wa Diamond, Babu Tale amesema Watanzania wengi bado tuna ushamba wa kujua maendeleo yaliyofanyika nchini na badala yake tumebaki kushangaa ya wenzetu.

Dar es Salaam. Meneja wa msanii Abdul Naseeb 'Diamond', Babu Tale amesema Watanzania wengi bado ni washamba na maendeleo yanayofanyika nchini.
Babu Tale amesema hayo jana Alhamisi katika ziara ya kutembelea ujenzi wa mradi wa reli ya umeme (SGR) ambayo ilijumuisha wasanii mbalimbali.
Tale amesema ni jambo zuri alilolifanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, PaulMakonda, kuwaandalia ziara hiyo ili wakajionee ujenzi  unavyofanyika kwa macho yao badala ya kusubiri kusimuliwa na kuongeza kuwa Watanzania walio wengi ni washamba wa kuyajua maendeleo waliyonayo.
"Kwa mfano Mimi nimezunguka katika nchi mbalimbali nimeona usafiri wa treni za umeme unavyofanya kazi jambo ambalo niliona sisi hatuwezi, lakini Rais John Magufuli ametuonyesha kuwa tukiamua tunaweza katika mradi huu,"alisema Babu Tale
"Uzuri zaidi tumeelezwa kuwa ujenzi wote umetokana na fedha zetu, hili linatia moyo na kama Watanzania hatuba budi kujivunia kulipa kodi matumizi yaketunayaona."
Awali, Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa aliwataka wasanii waliofanikiwa kutembelea mradi huo kusimama kifua mbele kutangaza kwa kuwa ni miaka 120, nchi  haijawahi kujenga reli.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametaka wasanii hao kuwapuuza wanaowabeza kuwa wamenunuliwa ili kufanya ziara hiyo.
Makonda amesema tatizo analoliona kuna changamoto ya utaifa kwa wananchi na kuwataka watu kuitumia mitandao kutangaza maendeleo yanayofanywa katika nchi hii.