Uhuru Suleiman aitamani tena Sauzi

Muktasari:

Uhuru Suleiman alizichezea klabu tofauti kabla ya kujiunga na Biashara United msimu huu. Alizichezea timu za Mtibwa Sugar, Coastal Union, Simba, Mwadui FC na Jomo Cosmo ya nchini Afrika Kusini.

Dar es Salaam.  Mshambuliaji wa Biashara United, Uhuru Suleiman yuko jijini Dar es Salaam akiendelea na mipango mingine ya safari atimkie Afrika Kusini na amesisitiza mguu uliokuwa ukimsumbua umepona.

Uhuru ambaye alitokea Afrika Kusini alikocheza kwa takribani miaka mitatu Klabu ya Jomo Cosmo na aliporudi alisajiliwa na Biashara United msimu huu, lakini ameshindwa kutamba kutokana na maumivu ya kifundo cha mguu.

"Nilikuwa nina tatizo la kifundo cha mguu ndiyo maana mechi nyingi za Biashara United sikucheza lakini sasa naendelea vizuri na tatizo langu limepona kabisa,"alisema Uhuru.

 "Hata hivyo nimewasiliana na wakala wangu amenambia kuna mpango wa kurudi tena Afrika Kusini kuna timu nitakwenda kucheza. Nitakuwa nasubiri huo mpango kuona tunafanikiwa vipi,"alieleza Uhuru na kufafanua mkataba wake na Biashara United haumzuii kwenda nje.

Hata hivyo, Meneja wa timu hiyo, Aman Josiah hakufafanua zaidi juu ya mchezaji huyo na badala yake alitaka atafutwe baadaye na alipotafutwa simu yake haikupokelewa.