Uhuru, Raila waungana na Wakenya kumpongeza Kipchoge

Muktasari:

Kipchoge, ambaye ni mshikilizi wa ubingwa wa Olimpiki, alitumia sekunde tisa mbele ya muda iliyowekwa na waandaaji wa mbio hizo za INEOS 1:59 Challenge, zilizomalizika muda mfupi uliopita Jijini Vienna, Austria

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani, Raila  Odinga wamewaongoza Wakenya kumpongeza, bingwa wa Dunia wa Marathon, Eliud Kipchoge baada ya kuweka rekodi ya kukimbia kilomita 42, ndani ya muda mfupi zaidi wa saa 1:59:40
Kipchoge, ambaye ni mshikilizi wa ubingwa wa Olimpiki, alitumia sekunde tisa mbele ya muda iliyowekwa na waandaaji wa mbio hizo za INEOS 1:59 Challenge, zilizomalizika muda mfupi uliopita jijini Vienna, Austria
Kabla ya kuanza kwa mbio hizo, Rais Kenyatta alimpigia Kipchoge moja kwa moja na kumtakia kila la kheri huku akiahidi kumpigia pindi atakapomaliza mbio hizo.
“Nitakupigia ukimaliza ndugu yangu, Mungu akubariki, utafanikiwa lakini kwetu sio mafanikio katika kuvunja rekodi bali pia kule tu kuthubutu ni mafanikio, kila la kheri ndugu yangu,” alisema Rais Kenyatta.
Kupitia akaunti yake ya Twitter, Waziri Mkuu wa zamani, Odinga aliandika: “Hata kabla ya kuanza kwa mbio hizi, tayari ulikuwa umeishangaza dunia, ulichokifanya ni zaidi ya uthubutu na ushujaa, Kongole sana kwa kumaliza mbio chini ya masaa mawili. Kenya imepata sifa!”
Makamu wa Rais wa Kenya,  William Ruto, alikuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza jijini Vienna, kumshuhudia Kipchonge akiushinda mkono wa muda.
Ruto, alionekana kwenye mstari wa watazamani wa kawaida, akifuatilia mbio hizo, ambazo zilimalizika kwa Kipchoge kuishangaza Dunia, alipoweka rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kumaliza Kilomita 42 ndani ya saa 1:59:40.
Mara baada ya mbio hizo kumalizika, ikiwa sekunde sekunde tisa mbele ya muda uliowekwa wa saa 1:59:49, Ruto alikuwa wa kwanza kwenda kumpongeza Kipchoge, kabla ya Wakenya na mashabiki wengine kutoka kila kona ya Dunia kuungana naye.