Uhamiaji yatwaa ubingwa netiboli

Tuesday September 11 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Timu ya Uhamiaji imeibuka bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Netiboli Taifa kwa kuweka rekodi tamu ya kutopoteza mechi yoyote kati ya tisa ilizocheza.

Ligi hiyo ilianza kutimua vumbi Septemba 4 kwenye viwanja wa CCM Kirumba Mwanza ikishirikisha timu 10 ambapo JKT Mbweni ndio walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo.

Awali timu 20 zilitakiwa kushiriki Ligi hiyo,lakini ni nusu yake tu ambayo iliweza kuthibitisha ushiriki wake,huku zingine zikitokomea mitini na sasa zitakumbana la kulipa faini ya Sh 1 milioni na nyingine kushushwa Daraja.

Katika michezo hiyo ilihitimishwa juzi Jumatatu, Uhamiaji kubeba taji kwa pointi 18 na kuwanyang’anya Mbweni JKT ambao walichukua nafasi ya pili kwa alama 16.

Magereza wao walishika nafasi ya tatu kwa pointi 14, Polisi Morogoro wakakaa nafasi ya nne kwa alama 12, Jeshi Star nafasi ya tano kwa alama nane sawa na Mgulani waliokaa nafasi ya sita kwa pointi nane.

Polisi Arusha waliishia nafasi ya saba kwa pointi saba, Arusha Queen wakasimama nafasi ya nane,Jiji Tanga nafasi ya tisa na mwenyeji Sedico wakaburuza mkia kwa kutopata pointi yoyote baada ya kuchezea vichapo tu.

Mchezaji Asha Said wa Jiji Tanga aliibuka mchezaji Bora wa mashindano hayo, huku Fatuma Matenga wa Uhamiaji akitangazwa kuwa mfungaji Bora.

Kocha wa Uhamiaji, Restuta Lazaro alisema kujituma kwa wachezaji wake na kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi ndio siri ya mafanikio yao na kwamba ushirikiano ni sababu nyingine.

“Kwa ujumla ushindani ulikuwa mkali lakini niwapongeze wachezaji wangu kwa namna walivyopambana na kuweza kufanikisha malengo yetu, kikubwa ni ushirikiano ndani ya timu,” alisema Lazaro.

 

 

Advertisement