Ugumu wa Ligi Kuu waivuruga Kagera Sugar

Muktasari:

 Kagera Sugar imechezea sare mfululizo katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba dhidi ya KMC na Ruvu Shooting, ambapo Oktoba 20 itakuwa ugenini kukipiga na Lipuli katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara. 

MWANZA. BAADA ya kufululiza sare katika mechi mbili kwenye uwanja wa nyumbani Kagera Sugar, Benchi la Ufundi limekiri Ligi kuwa ngumu kutokana na jinsi timu zinavyokamia kusaka ushindi.

Kagera Sugar ambayo imeshuka uwanjani mara nane bila kupoteza mchezo wowote,imevuna pointi 12 na kukaa nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ally Jangalu alisema kuwa licha ya kujipanga kushinda mechi zao za nyumbani lakini mambo yamekuwa magumu kutokana na Klabu kukamia kusaka matokeo mazuri.

Alisema kuwa tatizo katika safu ya ushambuliaji ndio iliwagharimu katika kushindwa kutumia nafasi vizuri walizopata na kwamba hata hivyo wanashukuru kwa kutopoteza mchezo hadi sasa.

“Ligi ni ngumu kila timu inajipanga kushinda bila kujali nyumbani wala ugenini,lakini tunashukuru kwa matokeo tuliyopata bila kupoteza na tutaendelea kupambana”alisema Kocha huyo.

Kwa upande wake Nahodha wa Klabu hiyo, George Kavila alisema kuwa kwa sasa wanajiandaa na mechi za ugenini wakianza na Lipuli kuhakikisha wanashinda.

Alisema kuwa kikubwa ni mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwasapoti ili kumaliza Ligi wakiwa katika nafasi nzuri na kwamba wamejipanga msimu huu kufanya kweli.

“Kwa sasa tunaenda kupambana mechi za ugenini kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,mashabiki wasikate tamaa waendelee kutusapoti ili kufanya vizuri na sisi tumejipanga msimu huu”alisema Mkongwe huyo.